WANAFUNZI WENYE UMRI WA MIAKA KATI YA 18 HADI 25 WATAHADHARISHWA MAHUSIANO YA KIMAPENZI SHULENI,VYUONI

Wanafunzi wenye umri wa miaka kati ya 14 hadi 25, wametahadharishwa kuhusu mahusiano ya kimapenzi shuleni na vyuoni na kutakiwa kuacha kwa kuwa ni moja ya sababu za mlipuko wa magonjwa ya afya ya akili.

Mtaalam wa afya ya akili na Msaikolojia tiba, Dk. Isaack Lema kutoka Chuo Kikuu cha sayansi ya tiba Muhimbili (MUHAS), ametoa wito huo akieleza mlipuko huo unatajwa kulikumba zaidi kundi hilo, akawataka kujiepusha na vichocheo vingine vinavyoweza kuwasababishia magonjwa ya afya ya akili.
Aidha, wamelishauriwa kujilinda na kufuata mtindo wa maisha ulio sahihi kitaalam kwa kufanya mazoezi na kula mlo unaozingatia maelezo ya kitaalam.

Maelezo hayo yanaonyesha kuwa katika sahani ya mlo, nusu iwe ni mbogamboga na matunda, robo protini na robo ni vyakula jamii ya wanga, hatua itakayowawesha wananchi kuepukana magonjwa yasiyoiambukiza, yanayotajwa kuchangia vifo vingi ulimwenguni, takwimu zikionyesha asilimia 34 ya vifo husababishwa na magonjwa hayo.

Kwa mujibu wa Dk. Lema, aliyekuwa akizungumza wakati akitoa elimu kuhusu afya ya akili katika ziara ya Mtandao wa Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), upimaji afya na elimu kwa wanafunzi zaidi ya 400 kwenye Chuo cha Afya cha Dar City College of Allied Science (CCoHAS) jijini Dar es Salaam, wanafunzi hawapawsi kuchanganya mahusiano ya kimapenzi na masomo.

Ziara hiyo ilishuhudia wanafunzi zaidi ya 115 kati ya 400 walipima afya zao ambapo wote walipata elimu kuhusu namna ya kujikinga ya magonjwa yasiyoambukiza, huku Meneja Mipango wa TANCDA, Happya Nchimbi akieleza kwamba, shirikisho hilo liataendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwawezesha kujua namna ya kuzuia na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Dk Lema ambaye kitaluma ni Mtaalam wa Afya ya Akili na Msaikolojia Tiba, alisema ni bora vijan na wanafunzi wakajiepusha wasichanganye masomo na uhusiano wa kimapenzi kwani tabia hiyo inaweza kuwaingiza kwenye matatizo ya afya ya akili.

“Uhusiano wa kimapenzi ni kichocheo cha magonjwa ya akili, hivyo ni muhimu kwa vijana na wanafunzi kuepuka, wasichanganye mambo hayo. Kwenda kinyume kunaweza kuwaingiza kwenye matatizo ya afya ya akili,” alisema Dk Lema, akaongeza: “Ni muhimu pia unywaji pombe na uvutaji bangi ukaepukwa, hivyo pia visababishi vyenye uhatarishi kwa mtu kupatwa na matatizo ya afya ya akili.”
Akifafanua, Dk. Lema alisema kuwa uhusiano huo wa kimapenzi unajumuishwa pamoja na masomo huweza kumsababishia mhusika kubadili tabia hata kujikuta ameangukia katika matatizo ya afya ya akili, hasa inapotokea katika uhusiano husika mambo hayaendi vizuri alivyotarajia au alivyozoea.
“Ukiwa ni mvulana, una uhusiano na binti darasani, bahati mbaya unayempenda baadhi ya masomo hayawezi, nawe huwezi kumsaidia, akaamua kwenda mtu mwingine mwenye uwezo nayo, ambaye ni mvulana, mkali wa masomo, bila kukushirikisha;

Binti akipata msaada mara mbili au tatu, anaanza kuwa karibu na anayemsaidia. Wewe mvulana ukabaini hilo unasituka na linaweza kukuchanganya kwa vile unampenda binti, mtaingia kwenye mgogoro. Mkifanikiwa kuutatua itatkuwa bahati yenu, ingawa uzoefu unaonesha wengi hushindwa kumaliza migogoro ya mahusiano. Hapo utapatwa matatizo ya afya ya akili,” alisema Dk. Lema.

Kuhusu visababishi vingine vya matatizo ya afya ya akili kwa wanafunzi, mtaalam huyo alieleza kwamba uvutaji wa bangi na unywaji pombe navyo husababisha mtumiaji wake kutoa tafsiri tofauti ya vitu au mambo, kinyume na hali halisi ilivyo, kutokana na ukweli kwamba kwa matumizi ya pombe na bangi, afya ya akili inakuwa imeathirika.

“Tuepuka pia pombe, nayo ni kisababishi chenye uhatarishi wa kupatwa na magonjwa ya afya ya akili. Hata bangi, ukiivuta na kwa akili yako ukamwona mwalimu kama sisimizi, maana yake itakuwa afya ya akili yako imeathirika hivyo tujiepushe na vihatarishi,” alisema Dk.Lema. 

Kwa mujibu wa Mhadhiri huyo wa Muhas, magonjwa ya afya ya akili huweza kusababisha mfadhaiko wa akili kwa vijana, ambapo ugonjwa wa sonona unaweza kusababisha mtu kusikia huzuni, kujaa mawazo, kujitoa kwenye mitandao ya kijamii, hata kujiona hawezi kufanya jambo fulani, hata kutaka kujiua.

Katika ushauri wake, mtalam huyo alisema ili kuepuka magonjwa ya afya ya akili ni lazima wanafunzi na vijana wajitambue thamani yao, pia kupima na kuchambua faida na hasara za mahusiano shuleni, pia zile za matumizi ya pombe na uvutaji bangi na wafanye uamuzi kutumia busara wakiangalia maisha yao ya baadaye.

Awali , muuguzi kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA), Elizabeth Likoko aliwataka wanafunzi hao kuachana na mtindo hatarishi wa maisha, badala yake kuzingatia kanuni za afya katika ulaji, akisisistiza matumizi kidogo ya chumvi na mafuta, pia sukari, akionya matumizi hayo yakizidi husababisha mtumiaji kupatwa na magonjwa sugu yasiyoambukiza ikiwamo saratani, kisukari, presha na magonjwa ya moyo.

Naye Mjumbe wa Bodi ya TANCDA, Waziri Ndonde ambaye ni mtaalam wa mazoezi, aliwashauri watanzania kujenga utamaduni wa kufanya kufanya mazoezi sahihi ili kujenga miili na kuilinda dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ambapo alisema Shirika la Afya Ulimwenguni,(WHO), linaelekeza kila mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 64 anapaswa kufanya mazoezi walau kwa dakika 30 kila siku.

Mtaalam wa afya ya akili na msaikolojia tiba, Dk. Isaack Lema ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili ( MUHAS), akitoa mada kwa wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi ya Tiba, City College of Health and Allied Science cha Dar es Salaam, kuhusu afya ya akili wakati wa semina na upimaji afya ulioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) chuoni hapo.
Wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi ya Tiba cha City College of Health and Allied Science wakipima afya baada ya kupata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.
Muuguzi kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) Elizabeth Likoko(kushoto) akitoa ushauri kwa mwanafunzi wa Chuo cha Afya naSayansi ya Tiba, City College of Health and Allied Science cha Dar es Salaam.

No comments: