Wafanyakazi Benki Ya NBC Wazipamba Mbio Za UDSM Marathon

 Mashindano ya mbio  za UDSM Marathon 2020 kwa mara nyingine yalishuhudia ushiriki mkubwa wakimbiaji kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wakati timu ya wafanyakazi wa benki hiyo walipojitokeza kwa wingi katika mbio hizo.

Zikipambwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, mbio hizo zilizofanyika mwishoni mwa wiki zilianza saa 12:00 asubuhi zikitoa fursa kwa washiriki kupitia kwenye vilima na viunga vyenye mandhari nzuri ndani ya chuo hicho. Mbio hizo zilihusisha umbali wa 21 Km (Half marathon), 10 Km  na matembezi ya 5 Km.

Pamoja na ‘kupasua’ vilima vilivyopo kwenye njia nzuri za chuo hicho washiriki pia walipita njia ya Sam Nujoma, eneo la Mlimani City ambapo shangwe na pongezi za wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara hizo zilikuwa kivutio na kuongeza ari miongoni mwa washiriki wa mbio hizo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi sambamba na kuwashukuru wadau na washiriki, Mh Kikwete alisema mbio hizo zinalenga kusaidia miradi mbalimbali ya Chuo hicho hususani ujenzi wa kituo cha wanafunzi ambacho kitaongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia ya wanafunzi.

"Hivyo basi ni fahari kubwa kwetu kuona mbio hizi zikiendelea kukua kwa mafanikio mwaka baada ya mwaka, na tunapenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kufanikisha ukuaji huu na kuzifanya mbio za mwaka huu kuwa na ubora usiosahaulika.’’ Alisema

Zaidi aliwashukuru wadau mbalimbali ikiwemo benki ya NBC kwa kuwa miongoni mwa wadau wakubwa wa mbio hizo.

Washiriki wote kutoka benki ya NBC walifanikiwa kukamilisha mbio zao ikiwemo km 5, km 10 na wengine km 21 na walipatiwa medali za kutambua jitihada zao hizo.

"NBC tunafurahi kwa mara nyingine kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizi " alisema Bw Theobald Sabi,  Mkurugenzi Mtendaji wa NBC. "Mashindano haya ni moja wapo ya mbio zinazojulikana zaidi nchini, na nadhani ni mafanikio mazuri kwamba washiriki wetu wote waliweza kumaliza  salama wakiwa na nguvu."

 Aliongeza, "NBC itaendelea kushiriki katika mbio hizi kwa namna zote, tukiwa kama washiriki na pia tukiwa kama mdau muhimu katika mbio. Mbali na uhusiano wetu madhubuti tulio nao na taasisi ya UDSM, ushiriki wetu katika mbio hizi unachagizwa pia na ajenda yake kuu ambayo ni kujenga kituo cha wanafunzi. ’’

Katika mbio hizo ilishuhudiwa mwanariadha kutoka Arusha Fabian Nelson wa Arusha akiibuka mshindi wa kwanza katika mbio za km 21 huku mwanariadha mwenzie kutoka pia mkoani humo Faulina Abdi akiibuka mshindi katika mbio za km 21 upande wa wanawake.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu Jakaya Kikwete (wa pili kulia) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili kushoto) sambamba na kutambua ushiriki wa benki hiyo katika kufanikisha mbio za UDSM Marathon zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Benki ya NBC ilikuwa ni moja wa wadhamini wa mbio hizo zilizolenga kusaidia miradi mbalimbali ya Chuo hicho hususani ujenzi wa kituo cha wanafunzi.

Viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiongozwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa William-Andey Anangisye (wa nne kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya wafanyakazi wa Benki ya NBC walioshiriki kwenye mbio hizo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw Theobald Sabi (katikati)


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu Jakaya Kikwete (Kushoto) akiongoza matembezi ya km 5 wakati wa mbio hizo. Wengine ni pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa William-Andey Anangisye (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Bw Theobald Sabi (katikati)

Timu ya wafanyakazi wa Benki ya NBC wakijipongeza sambamba na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw Theobald Sabi kwa kukamilisha mbio hizo

Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya NBC wakishiriki kwenye mbio hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw Theobald Sabi (wa pili kushoto) akimpongeza mmoja wa washindi katika mbio hizo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa William-Andey Anangisye (kushoto) akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC  Bw Theobald Sabi baada ya kukamilika kwa mbio hizo.  

Timu ya wafanyakazi wa Benki ya NBC wakijipongeza kwa kukamilisha mbio hizo.

No comments: