WABUNGE WATEULE KUAPISHWA LEO SAA KUMI
TAARIFA KWA UMMA
Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai (Mb) leo tarehe 08 Desemba, 2020 atawaapisha Wabunge wawili walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Tukio hilo litafanyika katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma saa 10:00 jioni.
Wabunge hao walioteuliwa tarehe 05 Desemba 2020 ni Dkt. Dorothy Gwajima ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akishughulikia Afya na Mhandisi Leonard Chamuriho ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika atawaapisha Wabunge hao kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (2)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020. Kanuni hiyo inaeleza kuwa endapo Mbunge atachaguliwa au kuteuliwa katika kipindi ambacho hakuna Mkutano wa Bunge unaoendelea, Spika atamwapisha katika eneo atakalolipanga na atatoa taarifa kwenye Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Bunge unaofuata.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA.
08 Desemba, 2020
No comments: