UDOM YAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI YA KUPAMBANA NA UTOVU WA MAADILI

CHUO KIKUU Cha Dodoma (UDOM) kimesema kitaendelea kupambana na changamoto ya rushwa ya ngono wanazokutana nazo wanafunzi wao kwa kukuza kiwango cha maadili kwa watumishi wake pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kupambana na utovu wa maadili.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili chuoni hapo, Dkt Ombeni Msuya ambaye amemuakilisha Makamu Mkuu wa Chuo hiko katika kikao kazi cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) leo jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa utafiti wa rushwa ya ngono uliofanywa na taasisi hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt Msuya amesema katika kukabiliana na changamoto ya rushwa ya ngono chuoni hapo wameanzisha madawati ya jinsia katika kila Idara zilizopo na kila Idara ikiwa na kiongozi wake jambo ambalo linawafanya wanafunzi wawe na sehemu ya kukimbilia wanapopata changamoto hiyo.

Amesema Chuo Kikuu cha UDOM pia kimeanzisha masanduku ya kutoa maoni kila mahali ndani ya Chuo hiko hasa katika Hosteli, Migahawani lengo likiwa ni kumuwezesha kila anaeona changamoto hiyo au vitendo hivyo vya utoaji rushwa ya ngono basi aweze kutoa taarifa ili taasisi iweze kushughulika nayo.

" Udom ni sehemu ya jamii, hivyo inawezekana wapo watu wachache wenye utovu wa nidhamu lakini wengi wanazingatia maadili. Chuo kinatoa pia elimu na hata jana tulikutana na wanafunzi wa mwaka wa kwanza na kuwajengea uelewa na elimu hii ya rushwa sambamba na kuwaambia umuhimu wa kutoa taarifa wanapopata hizo changamota.

Tumefungua pia madawati ya malalamiko kwenye maeneo mbalimbali ya Chuo chetu hadi kwenye Hospitali yetu lakini pia kuna Klabu ya wapinga rushwa UDOM ambayo ina miaka 10 hadi sasa, klabu hii ina wanafunzi, viongozi na watumishi na imekua msaada mkubwa sana katika kudhibiti na kuzuia vitendo hivi vya rushwa ya ngono," Amesema Dkt Msuya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM, Dk Ombeni Msuya akizungumza na wanahabari namna ambavyo Chuo hiko kimejipanga kupambana na utovu wa maadili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha UDOM ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chuo hiko, Dkt Ombeni Msuya akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma.
Wadau na wandishi mbalimbali wakimskiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM, Dkt Ombeni Msuya.
 

No comments: