TOZO ZISIZO RAFIKI KUKUZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KUONDOLEWA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto)
akifuatiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul
wakipatiwa maelezo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, namna ya kufuga samaki
kwa njia ya vizimba wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Ndaki katika
Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza,
kujionea namna mwekezaji Shamba la Konga anavyofuga samaki kupitia
vizimba ndani ya Ziwa Victoria.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akizungumza na
baadhi ya wavuvi katika Kata ya Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega
Mkoani Simiyu akiwataka watu wanaondelea kujihusisha na uvuvi haramu
kuacha mara moja vitendo hivyo na kubainisha ni wakati sasa jamii
kushirikiana na serikali kuwabaini watu wanaojihusisha na uvuvi haramu
kwa kuwa wanaishi katika maeneo wanayofahamika ili serikali ichukue
hatua.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akishuhudia na
kuhesabu idadi ya vizimba vya kufugia samaki vilivyopo ndani ya Ziwa
Victoria katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani
Mwanza, ambavyo vinamilikiwa na Shamba la Konga na kuwataka wananchi
wa kijiji hicho kuanza kufuga samaki ili wajiongeze kipato kwa kuwa
mahitaji ya soko la samaki yanayongezeka na kutaka kuanzishwa kwa
vizimba vya mafunzo katika kijiji hicho kupitia Wizara ya Mifugo na
Uvuvi.
Na Edward Kondela
SERIKALI imesema inatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia
tozo zote za mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na kuondoa tozo ambazo
zinakwamisha sekta hizo zisikue.
Akizungumza jana (30.12.2020) na baadhi ya wavuvi katika Kata ya
Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, wakati wa ziara
yake ya siku moja mkoani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki amesema wizara itaangalia tozo ambazo zitakuwa rafiki kwa
wawekezaji, wafanyabiashara pamoja na wafugaji na wavuvi wa hali ya
chini ili kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinachangia kwa sehemu
kubwa pato la taifa.
“Tutaenda kuangalia ni tozo zipi na baadhi tayari mmeshazitaja
zikiwemo za kusafirisha mazao ya mifugo na uvuvi nje ya nchi halafu
tunatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia hizi tozo zote.”
Amesema Mhe. Ndaki
Waziri Ndaki ambaye amefuatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe.
Pauline Gekul ameongeza kuwa uwepo wa tozo ambazo zitakuwa rafiki
katika kukuza sekta za mifugo na uvuvi kutasababisha watu wengi
kuwekeza katika sekta hizo na kuongeza pato la taifa kwa kuwa shughuli
za kuchumi zitaongezeka.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul
ameendelea kusisitiza kuwa watu wanaondelea kujihusisha na uvuvi
haramu kuacha mara moja vitendo hivyo kwa kuwa wizara haitafumbia
macho ambao bado hawataki kuacha kuharibu mazao ya uvuvi kupitia
vitendo hivyo.
Amesema ni wakati sasa jamii kushirikiana na serikali kuwabaini watu
wanaojihusisha na uvuvi haramu kwa kuwa wanaishi katika maeneo
wanayofahamika ili serikali ichukue hatua na kwamba Wizara ya Mifugo
na Uvuvi itazidi kutoa elimu juu ya athari ya uvuvi haramu kwa jamii
na taifa kwa ujumla.
Siku moja kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Simiyu, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wakati akihitimisha ziara ya siku
mbili Mkoani Mwanza amefika katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo
Wilaya ya Magu mkoani humo na kuzungumza na jamii ya wavuvi na
kuwasisitiza waanze kufuga samaki kupitia njia za vizimba na mabwawa
ili kujiongezea kipato na kuongeza kuwa mahitaji ya soko la samaki kwa
sasa ni makubwa.
Mhe. Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah kuhakikisha anaanzisha
utaratibu wa kuwepo kwa kizimba cha mafunzo kwa ajili ya kufugia
samaki na kuhakikisha wataalamu kutoka wizarani wanafika katika kijiji
hicho kuwafundisha wananchi namna ya kufuga na kulisha samaki ili
jamii ya hapo iweze kupata mapato kupitia mazao ya uvuvi.
Waziri Ndaki amebainisha hayo baada ya kutembelea vizimba vya kufugia
samaki katika kijiji hicho vinavyomilikiwa na Shamba la Konga na
kufurahishwa na namna mwekezaji anavyofuga samaki kwa wingi kwa njia
ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria kwa kuwa ni sera ya serikali
kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitano ajira zaidi ya elfu
arobaini na tano zinapatikana kupitia ufugaji wa samaki.
Katika kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Kitongosima wananufaika
kupitia ufugaji wa samaki Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Magu Bw. Lutengano Mwalwiba amewataka wanakijiji hao kujiunga
katika ushirika ili halmashauri hiyo iweze kuwakopesha fedha kwa ajili
ya shughuli za uvuvi huku Mwenyekiti wa Chama cha Wafuga Samaki Ziwa
Victoria Bw. Cyprian Matembo amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki kuangalia namna wizara inavyoweza kuwasaidia kupata
vyakula vya samaki kwa bei nafuu kwa kuwa kwa sasa vyakula vingi
vimekuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi na kuongeza gharama za
uzalishaji.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki leo (31.12.2020)
anahitimisha ziara ya kikazi katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa
kwenye Mkoa wa Shinyanga, baada ya kufanya ziara kwenye mikoa ya
Mwanza na Simiyu, akiambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe.
Pauline Gekul.
No comments: