TCRA, UCSAF WATEMBELEA KIJIJI CHENYE CHANGAMOTO YA MAWASILIANO


Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Godfrey Simbeye akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiana na Changamoto ya Mawasiliano katika kijiji cha Matuli,Ngerengere mkoani Morogoro wakati Bodi hiyo,TCRA walipotembelea kijiji hicho.
Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Lawi Odiero akizungumza na waandishi wa Habari wakati  ziara ya Kijiji cha Matuli, Ngerengere mkoani Morogoro chenye changamoto ya mawasiliano.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Matuli, Ngerengere mkoani Morogoro  Salum Ally  akizungumza namna  wanavyopata changamoto ya mawasiliano katika kijiji hicho.
Mti ambao unatumika katika kupata mawasiliano ya simu katika kijiji cha Matuli, Ngerengere mkoani Morogoro.
Mjumbe wa Bodi ya UCSAF Francis Chacha akizungumza kuhusiana na changamoto ya mawasiliano katika kijiji Matuli,Ngerengere mkoani Morogoro.

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV

 WAJUMBE wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wametembelea kijiji cha Matuli, Kata ya Matuli, Ngerengere, Mkoani Morogoro chenye changamoto ya mawasiliano na  kutoa hatua watazozichukua.

Wajumbe hao wa Bodi ya UCSAF walifika baada ya kupewa taarifa na Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Lawi Odiero ambaye alifanya ziara katika eneo hilo na kuona changamoto ya mawasiliano katika kijiji cha hicho kilichopo wilaya ya Morogoro vijijini.

Mtendaji wa Kijiji cha Matuli, ndugu Rashidi Ponera amesema kuwa wananchi wamekuwa wakipata adha wakitumia usafiri sh.5000 kufuata mti ili kuweza kupiga simu na huku mawasiliano siyo ya siri kutokana na kuweka sauti ya juu kukiwa na watu wengine.

Amesema kuwa hakuna mtu maalum aliyegundua mawasiliano ila mtu akifika kwenye mti anapata mawasiliano ndipo wakaweza kuita mti wa ajabu.

Mjumbe wa Bodi wa Godfrey Simbeye amesema kuwa kutokana na utaratibu wa Serikali  wa manunuzi ni baada ya miezi tisa watakuwa wamekamilisha ujenzi au katika suala la dharula ni ndani ya miezi sita.

Simbeye amesema kuwa Serikali iko katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za mawasiliano  hivyo watahakikisha bodi wanaotoa ushauri katika kufanikisha suala hilo.

Naye Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Lawi Odiero amesema kuwa baada ya kuona taarifa ya vyombo vya habari walifanya ziara na kuweza kuungana na UCSAF.

Mhandisi Odiero amesema kuwa suluhisho litapatikana ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano na Maendeleo mengine yanayotokana na mawasiliano.

"Tumepita hapa nia kuona changamoto ya mawasiliano huku Taasisi nyingine ya Serikali kuchukua na kufanyia kazi suala hilo kwa kuwa mawasiliano ni muhimu katika maendeleo ya nchi." amesema Mhandisi Odiero.

No comments: