Mngereza kuzikwa leo, Waziri Kuongoza Waombolezaji Kumuaga
Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dar es salaam
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa atawaongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, aliyefariki Desemba 24, 2020 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipokuwa anapatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na BASATA na familia, mwili wa marehemu Mngereza utawasili viwanja vya Karimujee jijini Dar es salaam kesho Jumanne Desemba 29, 2020 saa 3:20 asubuhi.
Mara baada ya mwili wa marehemu kuwasili katika viwanja hivyo, pamoja na taratibu nyingine za mazishi, kutakuwa na ibada fupi ya kumuombea, salamu za rambirambi pamoja na nyimbo maalum za maombollezo kutoka kwa wasanii na vikundi vya sanaa watakaoimba kumsindikiza kiongozi huyo.
Pamoja na Mhe. Waziri Bashungwa, watakuwepo pia viongozi mbalimbali wa Serikali, familia, watumishi wa Wizara na taasisi ya BASATA, wasanii, wadau wa tasnia ya sanaa, ndugu, jamaa, marafiki na baadaye safari ya kuelekea Suji wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro itaanza ambapo mwili wa mrehemu Mngereza utazikwa Jumatano, Desemba 30,2020.
Marehemu Mngereza atakumbukwa kwa umahiri wake mkubwa wa kuisimamia Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 1984 na Kanuni zake na uwezo wake wa kusimia maadili katika kazi za Sanaa pamoja na kuifahamu sekta kwa mapana yake hatua iliyosaidia kukuza maendeleo na utengenezaji wa kazi za Sanaa nchini zenye kujali ubora na maadili.
No comments: