Miaka 59 ya uhuru Kutoka Km360 hadi zaidi ya Km 14,000


Na Jonas Kamaleki

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazopiga hatua kubwa kiuchumi tangu kupata uhuru wake miaka 59 iliyopita.

Kwenye miundombinu ikiwemo ya barabara na madaraja, Tanzania imepiga hatua ya kupigiwa mfano, kwani wakati Tanganyika inapata uhuru barabara za lami kuunganisha mkoa na mkoa, wilaya na wilaya zilikuwa kilomita 360 tu wakati kwa sasa barabara hizo ni zaidi kilomita 14,000.

Upande wa elimu kwa mujibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wakati akizungumza katika sherehe za miaka 58 ya uhuru alisema wakati Tanganyika inapata uhuru shule za msingi nchini zilikuwa 3100 na kwa sasa ni zaidi ya 17379, za sekondari zilikuwa 41 tu kwa sasa ni takriban 4817.

Haya ni maendeleo makubwa kwa kipindi cha miaka 59 ya uhuru. Na hii inaonesha jinsi nchi inavyojiimarisha kiuchumi, miundombinu , elimu na afya vitazidi kuboreshwa.

Elimu ya juu imezidi kuboreshwa kwa kuongeza vyuo vikuu na wataalaam wanaofundisha vyuo hivyo kuongezewa ujuzi katika nyanja mbalimbali. Wakati Tanganyika inapata uhuru kulikuwepo chuo kikuu kimoja na hivi leo vipo vyuo vikuu 48.

Madaktari wazawa wakati Tanganyika inapata uhuru walikuwa 12 tu, kwa sasa nchi hii ina madaktari wazawa takriban 9400. Madaktari hawa kati yao wapo madaktari bingwa kwa fani mbalimbali wakiwemo wa upasuaji wa moyo, upandikizaji figo, magonjwa ya akina mama na mabingwa wa watoto. 



No comments: