MBUNGE LUDEWA AFANYA ZIARA NA VIONGOZI KUKAGUA KERO YA UBOVU WA BARABARA NA KUITAFUTIA UFUMBUZI
Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Kutokana na kilio Cha muda mrefu cha wananchi wa kata ya Madilu pamoja na Milo, juu ya ubovu wa barabara hatimaye kilio chao kimesikika baada ya Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kufanya ziara akiwa na viongozi mbalimbali kwa lengo la kukagua barabara hizo.
Barabara hizo ni kutoka Lusitu kupitia Madilu, Ilininda ambayo inaunganisha na kata ya Mundindi, pia na barabara ya Kigasi kupitia Milo, Ludende mpaka amani kuunganisha barabara ya Muholo, Mkongobaki na Lugarawa.
Mbunge huyo amefika katika maeneo hayo akiwa na mratibu wa Wakala wa barabara za vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Njombe Ibrahim Kibassa, Mkandarasi wa Wilaya hiyo Butene Jilala huku wakiongozana na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratius, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wise Mgina pamoja na watendaji mbalimbali wa serikali.
Amesema ameamua kuwapeleka viongozi hao ili kuona ni jinsi gani wanaweza kutatua tatizo hilo kwa muda wakati wakiweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo kwakuwa wananchi wa maeneo hayo walimpigia simu na kulalamika kuwa wanashindwa kusafirisha mazao yao kutokana na mvua zinazonyesha na kuharibu miundombinu ya barabara.
"Nilipigiwa simu na wananchi wakiniomba niwasaidie juu ya tatizo la barabara hasa katika kipindi hiki cha mvua kwakuwa wanashindwa kusafirisha mazao yao ya biashara, nikaona ni jambo jema kuwasaidia wananchi wangu ukizingatia maeneo haya yanajihusisha Sana na masuala ya kilimo cha biashara kama mbao, viazi, chai, na mengineyo", Alisema Kamonga.
Aliongeza kuwa katika barabara ya Lusitu mpaka Mundindi wameshindwa kukagua maeneo yote ambayo ni korofi kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha na kupelekea magari kushindwa kupita katika barabara hiyo ambapo iliwalazimu kuishia katika eneo la Mkelenge mpakani mwa kijiji cha Ilawa na Madilu.
Hata hivyo viongozi hao wa TARURA wameahidi kuchukua hatua za haraka kwa kutoa tenda kwa wakandarasi kupitia vikundi vilivyosajiliwa ili viweze kufanya matengenezo ya muda ambayo yatawawezesha wananchi hao kuendeleza shughuli zao.
Mratibu wa TARURA mkoani humo Ibrahim Kibassa amesema utekelezaji wa suala hilo utaanza wiki ijayo ambapo ndani ya wiki hii watafanya utaratibu wa kutoa mikataba kwa wakandarasi hao.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 serikali imetenga zaidi ya Bilioni 8 kwaajili ya ujenzi wa barabara mbalimbali za wilaya za mkoa huo ambapo kwa wilaya ya Ludewa imetengwa bilioni 1.2 .
"Tayari mkandarasi amesha patikana kwaajili ya ujenzi wa barabara mbalimbali za Ludewa na alitakiwa kuanza kazi kipindi hiki ila kutokana na hali ya mvua kwani atakapofanya ujenzi katika hali hii inaweza kuharibu zaidi miundombinu hiyo", Alisema Kibassa.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratius amesema matengenezo ya barabara hizo yatakuwa ni chachu ya maendelo ya wananchi kwa ujumla, mtu mmoja mmoja pamoja na halmashauri kwani kupitia biashara hizo za mazao zinazosafirishwa halmashauri itakusanya mapato ambayo yataleta Maendeleo katika wilaya hiyo.
" Hivi karibuni nilikutana na vijana wanaolima vitunguu wakalalamika kuwa vitunguu vyao vinaoza kutokana na kushindwa kusafirisha kwa wakati, hivyo naamini barabara hizi zikitengenezwa zitakuwa msaada mkubwa kwa wakulima na wafanya biashara", Alisema Deogratius.
Sanjari na ziara hiyo ya ukaguzi wa barabara, mbunge huyo ameendelea na zoezi lake la kugawa jezi kwa timu mbalimbali za vijiji zilizopo kwa kila kata, ambapo kila timu imepewa jezi 15 pamoja na mpira mmoja.
Mbunge wa jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga akiongea na wananchi wa kata ya Madilu (hawapo pichani) baada ya kushindwa kufika maeneo korofi kutokana na kutopitika. Kushoto ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Ludewa Sunday Deogratius na kulia ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wise Mgina (Diwani wa Mundindi)
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto)akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakikagua moja ya maeneo korofi katika kata ya Milo. Kushoto ni Mhandisi wa TARURA wilaya ya Ludewa Butene Jilala, mratibu wa TARURA mkoa wa Njombe Ibrahim Kibassa, mkurugenzi wa halmashauri ya Ludewa Sunday Deogratius, mwenyekiti wa halmashauri ya Ludewa Wise Mgina pamoja na Diwani wa kata ya Milo Robert Njavike. Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) akiwa sambamba na viongozi wa serikali katika zoezi la kukagua maeneo korofi katika barabara Lusitu mpaka Ilininda.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (aliyeshika mpira)akiwa kwenye picha ya. Pamoja na vijana wa kijiji cha Ikalo baada ya kuwakabidhi jezi 15 pamoja na mpira mmoja
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (Mwenye miwani) akigawa jezi kwa vijana
No comments: