KIBINDU YATARAJIA KUONDOKANA NA UKOSEFU WA MAJI SAFI-KIONAUMELA
………………………………………………………………………..
MWAMVUA MWINYI,PWANI
WAKAZI wa Vijiji ,Kata ya Kibindu, jimbo la Chalinze, Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanatarajia kuondokana na shida ya ukosefu wa maji safi na salama,inayowakabili kwa muda mrefu.
Taarifa ya James Kionaumela Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mzingira Vijijini (RUWASA), katika ziara katika vijiji vya Kibindu, Kwamduma, Kwamsanja na Kwakonje, inaeleza, utekelezaji wa miradi hiyo Serikali imetoa kiasi cha sh. Bilioni 1.6 ambapo milioni 700 kwa ajili ya Bwala la Kijiji cha Kwamsanja na Kijiji cha Mjembe kuna milioni 900.
“Kijiji cha Kibindu kina wakazi 11,154 wanapata maji kupitia mradi uliofadhiliwa na JIC mwaka 2009, vyanzo vyake visima viwili kila kimoja kina uwezo wa kutoa lita 6,000 kwa saa, unatumia Jenereta mbili una vituo 20 huku wateja 40 wameunganishiwa watu 10,238,” ilieleza taarifa hiyo..
Kionaumela alieleza, upanuzi wa mradi utaongeza mtandao wa bomba lenye urefu wa mita 830 kuelekea Vulala, shule ya Sekondari Kibindu na ujenzi wa vituo viwili vya kuchotea maji, na ufungaji wa pampu ya kutumia nguvu ya jua sanjali na ujenzi wa tenki dogo lenye ujazo wa lita 22,000.
“RUWASA kushirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu wamefanya upimaji hali ya upatikanaji wa maji ya chini ya ardhi, taarifa ya awali imewasilishwa na kuainisha maeneo ya uchimbaji wa visima, hatua inayofuata ni uchimbaji ili kupata vyanzo vya huduma,” ilibainisha Kionaumela.
Nae mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,Zainab Kawawa aliishukuru Serikali kwa kuweka kipaumbele katika miradi ya maji ambayo ndio changamoto kubwa.
Aliwataka viongozi wa RUWASA kutekeleza majukumu yao mapema ili kazi hizo zikamilike hatimae wanancji wanufaikea na huduma.
“Wakati anazungumza na Taifa kupitia ufunguzi wa bunge, Rais Dkt. John Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kuelekeza nguvu katika kutatua kero za wananchi, hususani sekta ya maji, leo tunashuhudia kazi inayofanyika, niwaombe hii kazi ikamilike mapema,” alisema Kawawa.
Mbunge wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete alifafanua,kero ya maji katika vijiji vinavyounda Kata ya Kibindu ilikuwa kubwa, na kwamba pamoja na uwepo wa mikakati hiyo wananchi walikuwa wanalalamikia ujenzi wa mabwawa hayo, lakini amepata faraja kubwa kuona RUWASA wakiwa katika harakati hizo.
“Wananchi wetu wa Kata ya Kibindu kwa muda mrefu walikuwa wanasubiri ujenzi wa mabwawa haya kwa ajili ya upatikanaji wa maji, leo nimefarijika sana kuona mikakati iliyopo ya kuwaondolea adha ya maji wananchi hawa,” alisema Ridhiwani.
No comments: