ZUCHU ALAMBA SHAVU DARLING HAIR
Yassir Simba, Michuzi TV
MALKIA wa muziki wa bongofleva kutokea katika label ya muziki ya WCB leo tarehe 19 mwezi Novemba amelamba Shavu dodo la kuingia ubalozi na kampuni ya kutengeneza nywele za kike ya Darling Hair huku mkataba na thamani yake hilo vikibaki kuwa siri kati ya msanii Zuchu na kampuni ya Darling.
Msanii huyo ambaye ana muda wa miezi tisa tu katika kiwanda cha muziki wa bongofleva amedai kuwa tangu alipoanza kutoa kazi zake za muziki chini ya WCB amekuwa akitumia nywele za kampuni hiyo katika kunogesha urembo wake huku pia kampuni hiyo ya Darling ikisisitiza kuwa kutokana na mafanikio ya haraka aliyoyapata msanii huyo Zuchu katika muda mfupi ikiwemo kuchukua tuzo ya msanii bora chipukizi barani Afrika katika Tuzo za Afrimma imewafanya wao kama kampuni kumuona msanii huyo kama balozi mzuri katika kutangaza bidhaa zao.
Mmoja wa mameneja kutoka WCB, Salam amewashukuru kampuni ya Darling kwa kumuamini msanii Zuchu kuwa balozi wao huku akisema kutokana na Zuchu kupata mafanikio katika muziki wake ndani ya muda wa miezi tisa katika muziki imeonyesha ni jinsi timu nzima ya WCB inavyofanya kazi kwa badii kufikisha muziki wa Tanzania mbele zaidi huku akiahidi kuwa hivi karibuni watatambulisha msanii mwengine mpya katika label yao.
Msanii Zuchu pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru mashabiki wa muziki kutoka Tanzania na kwengineko barani Afrika kwa kumuamini na kumpigia kura katika tuzo za Afrimma na kuibuka mshindi katika kipengele cha msanii bora chipukizi barani Afrika kwa mwaka 2020.
No comments: