ZAIDI YA WANAWAKE 2000 WAFANYIWA UKATILI MKOANI ARUSHA
Na Woinde Shizza , Michuzi Tv Arusha
JUMLA ya wanawake na watoto 2558 wamefanyiwa ukatili mkoani Arusha sawa na ongezeko la 22% kutoka mwaka 2918/2019 ambapo ukatili kwa watoto ulikuwa jumla 988.
Akizindua kampeni ya siku 16 za kuzuia ukatili wa kijinsia Jana mkuu wa mkoa wa Arusha Iddy Kimanta alisema idadi imeongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka huu ambapo kutoka idadi ya watoto 988 mwaka 2018/2019 idadi imepanda hadi kufikia 1256 kwa watoto.
"Mwaka huu idadi ni kubwa naamini nikiendelea kuwepo mwakani tunatamani kuwa kati ya mikoa ambayo ina idadi ndogo au kutokuwepo kabisa kwa ukatili wa wanawake na watoto" Alisema Kimanta.
Alisema tabia za ukatili wa kijinsia zimekuwa zikiathiri na kupelekea madhara makubwa katika familia nyingi ambapo alisema wakina mama na baadhi ya kina baba wanaathiriwa na ukatili huu kutokana na watoto wao kufanyiwa vitendo hivyo.
Alitoa rai kwa wadau mbalimbali kuwajengea uwezo watoto wa kuweza kuripoti pindi wanapofanyiwa ukatili huu akidai kuwa watoto wanapofanyiwa hayo wanakosa ujasiri wakuweza kutoa taarifa na kubaki na maumivu ya moto kwa muda mrefu.
"Watoto wengine hulazimika kuacha shule, kukimbia katika familia zao,kupata ulemavu,wengine kujikuta ndoa za utotoni pamoja na viwango vya ufaulu kushuka lakini matukio yote haya yanatokea katika jamii zetu na baadhi ya jamii hunyamazia bila kutoa taarifa" alisema.
Alitoa maagizo ya kila mmoja katika nafasi yake kuhakikisha wanachukua hatua kuweka mazingira salama, majumbani, kazini, shuleni na hata mitaani na kutoa taarifa dawati la jinsia pindi yanapotokea matukio ya ukatili.
Uzinduzi huo umefanyika mkoani Arusha huku ukiudhuriwa na taasisi mbalimbali zinashughulika na maswala ya unyanyasaji wa kijinsia, wanafunzi wa shule mbalimbali za mkoani hapa, na kauli mbiu ya mwaka huu, 'Tupinge ukatili wa kijinsia mabadiliko yanaanza na Mimi'
No comments: