WAKUU WA WILAYA, WAKUU WA MIKOA TUMEANZA PAMOJA, TUTAMALIZA PAMOJA …CHAPENI KAZI-MAGUFULI

 *


Awaambia hana mpango wa kufanya mabadiliko yoyote

*Aweka wazi kwamba atalisuka upya baraza la Mawaziri

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

RAIS Dk.John Magufuli ameamua kuwatoa hofu wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa pamoja na watendaji wengine Serikali ambao wamekuwa na wasiwasi huenda wakaondolewa baada yay eye kuapishwa katika awamu ya pili ya uongozi wake.

Amewahakikishia kwamba hana mpango wa kubadilisha wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, watendaji wala mtendaji yoyote kwani kama mafanikio ambayo yamepatikana katika Serikali anayoingoza nao wanamchango wao na kama ushindi wa CCM wa asilimia 84 ambao wameupata katika Uchaguzi Mkuu nao wamehusika.

Dk.Magufuli amesema hayo leo Novemba 9, 2020 baada ya kumuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia nafasi za wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.

Wakati anazungumzia hilo, alianza kwa kueleza hivi“Nilitaka nichomekee tu hapa , pamekuwa na tabia kila serikali mpya inapoingia au awamu nyingine inapoingia watu wanakuwa na hofu hasa watendaji wa Serikali , kwamba wapatatokea mabadiliko , mabadiliko , mabadiliko.

“Na kwa sasa hivi naona wanahofu sana wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na ninashangaa kwanini wanakuwa na hofu , kwasababu kama ni mafanikio ya Serikali ni pamoja na wao , kama ni ushindi wa asilimia 84 ni pamoja na wao , ndio wamewezesha ushindi huo kupatikana kutokana na kazi ambazo wamefanya ya kuleta maendeleo katika maeneo yao.

“Wanasiasa ambao tumeguswa na hili, ni mimi Rais ambaye ilibidi niende kuomba kura pamoja na Makamu wa Rais, mwingine aliyeguswa ni Waziri Mkuu kwasababu lazima tuteue tena Waziri Mkuu , pamoja na Mawaziri, wengine nashaanga.Pia watakaoguswa ni Spika na Naibu Spika , kwasababu lazima wapigiwe kura wakishachaguliwa tutakuwa nao na wiki ya kupimwa ni hii.Mkuu wa Mkoa unakuwa na wasiwasi gani?

“Kama ulikuwa hufanyi kazi vizuri hapo sawa, maana napokea vimeseji, mheshimiwa Rais nimejitahidi katika kazi zangu , kana kwamba kipindi chake nilimwambia kinaisha baada ya mimi kuapishwa, nimeona hili nilizungumze kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya msiwe na wasiwasi na inawezekana isitokee mabadiliko hata moja.

“Labda kwa mtu atayekastaafu au kwa aliyefanya mambo ya hovyo sana, kwanini nibadili mkuu wa mkoa?Kwanini nibadilishe Mkuu wa Wilaya, kwanini nibadilishe mkurugenzi , kwanini nibadilishe DAS, Serikali ni ile ile , kama nilikuteua mwaka jana au miaka miwili mitatu au mitano iliyopita si uwezo bado ule ule na mtu ni yule yule.”

Akiendelea kuelezea hilo, Dk.Magufuli amesema kwa hiyo anajua inawezekana wanasikia,wachape kazi na wasipochaka kazi shauri yao , wakijiandaa kwamba wanaondoka basi, labda wao waandike barua ya kuondoka lakini yeye anajua alianza nao, atamaliza nao.

“Lakini ni hivyo hivyo kwa watendaji wengin , ninyi si mpo tu mnawasi wasi wa nini? Vyombo vya ulinzi na usalama ni vile vile sasa unabadilisha kitu gani na ndio uliowaweka, makamu wa Rais ni huyo huyo , inawezekana na Spika akawa ni huyo huyo na Naibu Spika akawa ni huyo huyo , Mwanasharia Mkuu amekuwa ni huyo huyo ,na ninyi mtakuwa ni hao hao ,

“Niliona nilizungumze hili, hata Katibu Mkuu kiongozi ni huyo huyo, natoa mwito kwa watendaji wenzangu ndani ya Serikali wachapake kazi, kwasababu kuchaguliwa kwetu hakuna maana sasa tunakuja kubadilisha.

“Hata Gavana wa BoT maana na wewe ujiandae nibadilishe Gavana kwanini? Kwa hiyo watu wachape kazi katika nafasi zao , kwa maana nyingine hakuna mabadiliko, tulianza wote na tutamaliza wote , mabadiliko yatakayokuwepo ni kwa nafasi tu zile za Uwaziri na Naibu Waziri ambazo zenyewe tulikwenda kuomba upya.

“Wapo ambao watarudi, wapo ambao hawatarudi tena siku hizi options ni kubwa,kuna wabunge ni 264 kwa hiyo uchaguzi ni mkubwa zaidi , hili sitaki kusema uongo, nikishamaliza hili basi mambo yatakwenda sawasawa wengine wachape kazi tu, ndugu zangu niliona nizungumze hili kwamba watendaji ndani ya Serikiali chapeni kazi zenu,”amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza wapo na mtaendelea kuwepo, ila ikifika wakati wa kustaafu hilo ni suala jingine au ukiamua kuandika barua ya kuondoka hilo nalo ni suala lingine, au spidi ikiwa haiendani na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, lakini sasa hivi kila mtendaji katika kila mahali achape kazi.

“Makatibu tawala, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya,watendaji wa vijiji, watendaji wa kata, na watendaji wengine wote waliko kwenye utumishi wa Serikali wachape kazi, kwanza kila mwaka unafanya kazi ya kuapisha nayo inachosha, uapishe wakuu wa wilaya,uapishe wakuu wa mikoa, inachosha, tumeshamaliza, tumemaliza watu wachape kazi,”amesema Dk.Magufuli.

No comments: