"UCHAGUZI SASA UMEKWISHA." ASEMA RAIS MAGUFULI MARA BAADA YA KUAPISHWA
*Rais wa Uganda, Zimbabwe, Comoro watoa neno mbele ya maelfu ya Watanzania.
Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Dodoma
RAIS Dkt.John Magufuli amewaambia Watanzania Uchaguzi Mkuu umekwisha na sasa kinachotakiwa ni kuendelea na jitihada za kuleta maendeleo ya nchi yetu na kwamba ahadi zote ambazo wamezitoa kwa wananchi zitatekelezwa.
Akizungumza leo Novemba 5,2020, baada ya kuapishwa Dkt. Magufuli ameanza kwa kueleza siku kama ya leo ya Novemba 5 mwaka 2015 aliapishwa kuwa Rais na leo ameapishwa tena.
Amesema mwanzoni aliapishwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam lakini sasa ameapishwa uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma ambako ndiko yalipo makao makuu ya Serikali, hivyo amemshukuru Mungu.
"Nawashukuru watanzania kwa kuniamini na kunichagua tena kwa miaka mitano kuongoza nchi, Ushindi ambao nimeupata mimi na Chama changu ni Watanzania wote. Pia nawapongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kwa kusimamia na kuendesha uchaguzi mkuu vizuri."
"Pia nawashukuru viongozi wa dini kwa maombi,dua na sala katika kipindi chote cha mchakato ws uchaguzi mkuu.Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama na watanzania wote kwa kufanikisha uchaguzi kwa amani."amesema Dkt. Magufuli.
Amefafanua kuvuka salama Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni uthibitisho wa namna ambavyo Mungu analipenda Taifa la Tanzania na Watanzania. Uchaguzi mkuu ulikuwa mtihani mwingine kwa nchi yetu, tunashukuru tumevuka salama, nchi nyingine zimeingia kwenye machafuko kwasababu tu ya uchaguzi.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Magufuli ameweka wazi Uchaguzi mkuu sasa umekwisha.
"Uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi umekwisha,nasema uchaguzi umekwisha, sasa jukumu lililopo mbele yetu ni kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo ya nchi yetu."
"Kiapo ambacho nimeapa mimi na Makamu wa Rais tutaendelea kukilinda kwa ngvuvu zote.Tutaendelea kulinda amani,umoja na mshikamano, tutaendelea kuulinda Muungano na mapinduzi matukufu ya Zanzibar,"amesema Dk.Magufuli.
Kuhusu ahadi ambazo wamezitoa wakati wa kampeni, kupitia Ilani yenye kurasa 303 zote anazikumbuka na zote watazitekeleza. Pia amesema wataendelea kutatua kero na changamoto ambazo zinawakabili Watanzania na kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua kimaendeleo. Pia amesisitiza kuendelea kusimamia rasilimali za nchi yetu na kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Dk.Magufuli ameeleza kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mkuu mwingine.Kuhusu watu waliojitokeza uwanjani hapo kushuhudia tukio la kuapishwa kwake, amesema anawashukuru wote waliofika na wanaofuatilia tukio hilo na kwamba atahakikisha unajengwa uwanja mkubwa Dodoma ambao utachukua watu wengi, kwani leo watu wengi wamekuwa nje kutokana na udogo wa uwanja.
Wakati huo huo baadhi ya marais waliohudhuria tukio hilo wamempongeza Dk.Magufuli kuchaguliwa tena kuwa Rais kwa awamu ya pili ambapo Rais wa Uganda Yoweri Museven amesema "Kwa niaba ya wananchi wa Uganda tunatoa hongera kwa Rais Magufuli kushinda uchaguzi, pili tunatoa pongezi kwa CCM kwa kupata ushindi, tena kwa amani.
"Pia nawapongeza watanzania kwani miezi mitatu nyuma wameingia uchumi wa kati. Hata hivyo wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu nilikuwa nafuatilia muelekeo wa CCM maana hao wengine(wapinzani) sijui muelekeo wao.
"Chama Cha Mapinduzi kimebeba maana halisi ya ukombozi wa Afrika hasa baada ya Uhuru kwani ni viongozi wachache sana hasa Mwalimu Nyerere aliyebaki na uzalendo wa kweli na Kaunda na wengine wachache sana,"amesema Rais Museven.
Amesema uwepo wa viongozi mbalimbali wa Afrika katika sherehe za leo,ni uthibitisho wa kweli unatoa picha halisi ya Mwalimu Nyerere na wale viongozi wachache." Waasisi wetu walisimamia mambo manne ambayo ni ukombozi wa bara la Afrika, ustawi wa maendeeleo ya wananchi, usalama wa chakula na undugu." Amesema.
Kwa upande wa Rais wa Zimbabwe Emmason Mnangwaga amesema Wazimbabwe wanatoa pongezi nyingi sana kwa Rais Magufuli, na wanaitazama Tanzania kama baba na mama wa Uhuru wao na Mwalimu Nyerere wanamuangalia kama mzalendo wa kweli."Wakati wa kutafuta uhuru nchi za Afrika zilikuwa hapa Tanzania."
Pia amesema Zimbabwe wanamshukuru Dk.Magufuli alipokuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kuzitaka jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo vya kiuchumi."Tunakushukuru Rais Magufuli kwa tamko lile, lakini tunakumbuka ziara yako ulivyokuja Zimbabwe kwani pamoja na mambo mengine mlitusaidia msaada wa mahindi." amesema.
Wakati Rais wa Comoro Azan Othman ametumia nafasi kuwapongeza Watanzania kwa kufanikisha uchaguzi mkuu, pia amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuongoza Tanzania.
No comments: