TAKWIMU ZA UKATILI NA UDHALILISHAJI ZATOLEWA ZANZIBAR
Na Mwashungi Tahir
IMEELEZWA kwamba Wazazi na Walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili wanapofikwa na vitendo vya udhalilishaji waweze kuwaeleza baada ya kuonekana vitendo hivyo vinaongezeka Zanzibar kila siku.
Hayo ameyasema Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Khamis Mwinyi Bakar katika kikao na waandishi wa habari huko katika Ofisi ya Mtakwimu iliopo Mazizini wakati wa ikiwasilishwa takwimu za Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kwa wanawake na watoto.
Amesema wazazi wengi wanakuwa na tabia ya kupuuza taarifa za awali za udhalilishaji ambazo wanapewa na watoto wao jambo ambalo linapelekea vitendo hivyo kuzidi kukua zaidi hadi kuwaathiri.
“Tuwe na tabia ya kuwa karibu na watoto wetu ili kuwabaini kwa haraka pale wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kuvipatia ufumbuzi kwa haraka.” Alisema Khamis Bakari.
Akiwasilisha takwimu za udhalilishaji za mwezi Oktoba 2020 Mtakwimu kitengo cha Makosa ya Jinai, Madai na Jinsia Ramla Hassan Pandu amesema jumla ya matukio 103 ya ukatili udhalilishaji na jinsia yameripotiwa idadi ambayo inaonekana kushuka ukilinganisha na mwezi wa Septemba 2020 ambapo jumla ya matokeo 116 yaliyoripotiwa.
Amesema Wilaya ya Mjini imeripotiwa kuwa na matukio mengi zaidi ikilinganishwa na Wilaya nyengine ambapo matukio 29, ikifuatiwa na Magharibi ‘B’matukio 19, Wilaya ya Kaskzini “A” na Kusini ina idadi ndogo zaidi ya matukio kuliko zote matukio mawili kwa wilaya zote.
Aidha amesema takwimu zinazotolewa zinahusu aina za ya matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambayo yameainishwa katika matukio makuu sita ikiwemo kubaka,kulawiti,kuingiliwa kinyume na maumbile . kutorosha,shambulio la aibu/kukashifu na shambulio.
Nae Mkurugenzi wa wanawake na watoto kutoka Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na watoto Nasima Haji Chum amesema ni jukumu la wazazi kushirikiana katika suala la malezi il kuendelea kupunguza vitendo vya udhalilishaji.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mayasa Mahfoudh Mwinyi amewataka wadau wa maswala ya udhalilishaji kuhakikisha masuala ya udhalilishaji yanapungua ili kutimiza azma ya Serikali.
Mkutano huo ni endelevu ambao kila mwezi ripoti za udhalilishaji hutolewa ambapo imefuatana na miongoni mwa shamrashamra za kuelekea siku ya Takwimu za Afrika ambapo kauli mbiu ya mwaka huu.
Uboreshaji wa mifumo ya Takwimu kitaifa kwa uzalishaji wa Takwimu na utoaji wa Taarifa ili kuwepo kwa amani na Maendeleo endelevu Barani Afrika.
No comments: