TAASISI YA FURAHIKA YAZINDUA STUDIO YA MUZIKI, REKODI KUFANYIKA BURE



Afisa mnwandamizi wa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA,) Bonnah Masenge akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua studio hiyo ambapo amesema kuwa baraza hilo lipo tayari muda wowote  kuwahudumia wananchi huku maadili na nidhamu, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Furahika Education College David Msuya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na programu za mafunzo ya ufundi ukiwemo muziki zitakazotolewa bure na taasisi hiyo, amesema mpango huo ni katika kuunga mkono jitahada za Rais Dkt. John Magufuli katika ujenzi wa Taifa la viwanda, leo jijini Dar es Salaam.
Afisa mwandamizi wa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA,) Bonnah Masenge akikata utepe kuashiria uzinduzi wa studio hiyo inayoendeshwa na Taasisi ya Furahika ambapo vijana watapata fursa ya kupata mafunzo na kurekodi bila malipo, leo jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi wa kituo cha Furahika jijini Dar es Salaam wakitoa burudani wakati wa hafla ya uzinduzi wa Studio ya mafunzo na rekodi za muziki kwa vijana iliyopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wazazi na wakazi wa Buguruni Malapa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa studio ya mafunzo na rekodi za muziki katika kituo cha Furahika jijini Dar es Salaam. 


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA,) limeeleza kufurahishwa na hatua za Taasisi ya Furahika Education Centre iliyopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kwa kuzindua rasmi studio ya kurekodi na kutoa mafunzo ya muziki kwa vijana bila malipo yoyote jambo linalotoa fursa kwa vijana kujitengenezea kipato binafsi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua Studio hiyo Afisa sanaa mwandamizi kutoka BASATA Bonnah Masenge amesema, milango ya baraza hilo ipo wazi kwa kutoa huduma na ushauri huku maadili yakiwa ni kipaumbele.

Amesema, baada ya kukagua studio hiyo wameona kuwa sehemu hiyo ni kituo bora kwa vijana kujifunza na kujiajiri kupitia sanaa.

"Tunawaomba wadau watambue juhudi za namna hii na kuweza kuwasaidia vijana pamoja na kuleta mabadiliko katika sanaa ya muziki." Amesema.

Bonnah amewaagiza wasimamizi wa kituo hicho kuzingatia ubora na viwango kwa kuwa sekta ya muziki ni pana na yenye ushindani, hivyo ni vyema watayarishaji wawasaidie vijana kutoa muziki bora katika soko, wenye nidhamu na maadili.

Kwa upande wake Mkurugenzi na msimamizi wa kituo hicho David Msuya amesema, kituo hicho kimekuwa kinatoa elimu pamoja na kutetea haki za watoto mashuleni na hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika kujenga Taifa la viwanda.

"Fursa zipo muhimu ni elimu tuu na wasanii wengi hawana elimu ya muziki tunaamini kupitia mafunzo haya  sekta ya muziki itakua zaidi hasa katika kupambana na soko la ajira." Amesema Msuya.

Taasisi hiyo iliyosajiliwa na VETA inatoa mafunzo mbalimbali ya ufundi kwa kuchangia vitendea kazi pekee, huku mafunzo yanayotolewa katika kituo hicho yakijumuisha ufundi wa magari, Cherehani, Useremala, ujenzi, mafunzo ya hoteli, Kompyuta, urembo, mapambo pamoja na Muziki.

No comments: