SIMBA SC WATOA DOZI NENE ARUSHA
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Aghaa!!! Wambie Simba...Simba Kiboko yao, hivyo ndio unaweza kusema baada ya Mabingwa watetezi wa Michuano ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba kutoa dozi nene katika dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha baada ya kupata ushindi wa bao 7-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mtanange wa VPL uliopigwa kwenye dimba hilo.
Simba SC wametoa dozi hiyo kwa mabao ya Hassan Dilunga dakika ya 7 John Raphael Bocco dakika ya 24, 29, 38, Bernard Morrison dakika ya 45 na Clautos Chama dakika ya 61, 85.
Baada ya mchezo huo Nahodha wa Kikosi cha Simba SC, John Bocco amesema wametoa kipigo hicho kutokana na kujipanga vizuri kwa Kikosi chao na muelewano mzuri wa Wachezaji wenzake sambamba na kufuata maelekezo ya Kocha wao.
"Coastal Union ni timu nzuri, wamecheza vizuri pia, Kipindi cha kwanza na hata cha pili lakini makosa walifanya yamepelekea sisi kuwaadhibu mabao 7-0", amesema Nahodha Bocco.
"Kuhusu tuzo ya Ufungaji Bora bado tunapambana kwanza na timu, lazima tuhakikishe timu yetu inafanya vizuri kwanza katika Ligi na kufika mapengo, hapo ndio tutaangalia suala la Ufungaji Bora", ameeleza Bocco.
Naye Nahodha wa Coastal Union, Ally Salim Kipemba amesema walijitahidi kucheza vizuri lakini makosa waliofanya ndio hayo Simba SC wametumia kuwaadhibu mabao 7, amesema watajipanga na kufanya marekebisho yote ili michezo ijayo wafanye vizuri.
Simba SC wanafikisha alama 23 na mchezo 11 baada ya ushindi huo wakati Coastal Union wao wakibaki na alama zao 12 katika michezo 11 baada ya kipigo hicho. Simba SC wanajiandaa na mchezo wao wa Kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United ya Nigeria mchezo utakaopigwa kati ya Novemba 27, 2020 katika Jimbo la Jos nchini Nigeria wakati mchezo wa marudiano ukitarjiwa kuchezwa Desemba 4 jijini Dar e Salaam.
No comments: