SHIRIKA LA WOMEN@WEB LAZINDUA KAMPENI KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA DHIDI YA WANAWAKE, WASICHANA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII

Na Said Mwishehe, Michuzi TV


SHIRIKA la Women@Web nchini Tanzania limezindua kampeni maalumu ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana mitandaoni huku ikitolewa rai kwa jamii kuhakikisha inashirikiana na Serikali kupunguza au kumaliza kabisa ukatili huo.

Kwa mujibu wa Women@Web ni kwamba kampeni hiyo ya siku imeanza leo na miongoni mwa mambo yanayofanyika katika kipindi cha kampeni hiyo ni kuelimisha jamii kuwa na matumizi salama ya mtandao na kubwa zaidi kujiepusha na vitendo vya aina yoyote vinavyoashiria ukatili wa kijinsia mitandaoni hasa unaofanywa dhidi ya wanawake na wasichana.

Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 120 kutoka mashirika , taasisi pamoja na wanafunzi wa vyuo, Kiongozi Mwenza wa Shirika la Women@Web Carlo Ndosi amesema lengo la kampeni hiyo ni kupunguza ukatili wa kijinsia kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Amefafanua kuwa kampeni hiyo imelenga kuangalia tatizo la unyanyasaji wa kijinsi mtandaoni kama changamoto wanayokumbana nayo wanawake na wasichana imekuwa ikiathiri ushiriki wa wanawake mijadala mbalimbali mtandaoni, hivyo kuna kila sababu jamii kushirikiana kuondoa unyanyasaji huo mtandaoni.

"Kwa kutumia kampeni hii ambayo tumeizundua leo hii tutahakikisha tunatoa elimu ambayo itazungumzia umuhimu wa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa na matumizi salama ambayo hayana unyanyasahi wa kijinsia kwa wanawake na wasichana,"amesema Ndosi.

Aidha amesema nchini Tanzania kuna watumiaji wa mtandao milioni 27 kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) lakini kati ya hao haijulikani wanawake ni wa ngapi lakini wanafahamu kutokana na sababu za utamaduni na sababu za kielimu ushiriki wa wanawake ni mdogo zaidi kuliko wanaume.

"Kwa hiyo Women@Web tumejikita katika kutoa elimu inayohusu matumizi salama mtandaoni , tumejikita katika kuhamasisha watumiaji wa mitandao kuzingatia haki za watumiaji wengine wa mtandao.Hakuna sababu ya kutumia mitandano kunyanyasa wengine. Ni lazima watu watambue haki na wajibu,"amesema Ndosi.

Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Kupambana na unyanysaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana kutoka Shirika la UN Women Tanzania Lucy Tesha ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa jamii kushirikiana na Serikali yetu ili kuhakikisha suala la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo yote yanapunguzwa au kutokomezwa kabisa.

Amesema wanasisitiza hata wanaume hasa vijana kuwa makini katika matumizi salama ya mitandao na wanapenda kuona kunakuwa na machampioni ambao watawalinda wanawake na wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia mtandaoni.

Pia amesema ni muhimu kwa wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kunakuwa na takwimu sahihi na kufanyika kwa tathimini ambayo itasaidia katika kukomesha ukatili na unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni na kwenye jamii kwa ujumla.

Pamoja na mambo mengine washiriki wamepata fursa pia ya kupata elimu inayohusu matumizi sahihi ya mtandaoni kwa lengo la kuhakikisha kila anayetumia anajua wajibu wake.hata hivyo akieleza kuwa kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka huu wa 2020 zaidi ya wanawake 250 tayari wamepatiwa elimu ya matumizi salama ya mtandao na wanaendelea kuitoa kwa wengine. 


Kiongozi wa timu ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana kutoka Shirika la UN Women Tanzania Lucy(wa nne kulia) akiwa katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia mtandaoni uliofanyika leo jijini Dar es Salaan .Wengine ni washiriki kutoka mashirika na taasisi mbalimbali

Kiongozi Mwenza kutoka Shirika la Women@Web Asha Abinallah( wa kwanza kulia) akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ukatili wa kijinsia mtandaoni iliyoandaliwa na Shirika hilo.Pembeni yake ni Kiongozi Mwenza wa Women@Web Carlos Ndosi.



Kiongozi Mwenza wa Shirika la Women@Web Carlos Ndosi akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo



Sehemu ya washiriki waliohudhuria tukio hilo la uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia mtandaoni wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kuhusu namna nzuri ya kutumia mtandao kwa matumizi salama

Sehemu ya washiriki waliohudhuria tukio hilo la uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia mtandaoni wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kuhusu namna nzuri ya kutumia mtandao kwa matumizi salama



Baadhi ya washiriki wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia mtandaoni wakiwa wamesimama kuonesha ishara ya kuungana kupinga ukatili huo

Sehemu ya maofisa kutoka Shirika la Women@Web wakijadiliana jambo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ukatili wa kijinsia mtandaoni

Sylvia Mkomwa ambaye ni moja ya washiriki wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia mtandaoni akifafanua jambo wakati wa uzinduzi huo

Mwanachama wa Jeshi la dada Viola Julius ( kulia) akizungumza kwenye uzinduzi huo

Mkurugenzi Mtendaji wa Dexterous Mary Nsia Mangu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo

 

No comments: