SHAHIDI AANIKA WALIVYOKUTWA NAVYO WATUHUMIWA WA KESI YA DAWA ZA KULEVYA
Na mwandishi wetu, Dar es Salaam.
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama mahakama ya mafisadi imeelezwa kuwa, mshtakiwa Ayubu Kiboko na mkewe Pilly Mohamed wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 251.25 pia walikutwa na bastola moja na risasi saba.
Shahidi wa tatu wa upande wa Jamuhuri katika kesi hiyo, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Emmanuel Ambilikile ameeleza hayo leo Novemba 25,2020 mbele ya Jaji Lilian Mashaka wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Kanditi Nasua, Insp. Ambilikile amedai kuwa Mei 23, mwaka 2018 katika maeneo ya Tegeta jijini Dar es Salaam, waliwakamata washtakiwa hao ambapo wakati wa ukamatwaji mbali ya kukutwa na bastola na risasi pia walikamata kiboksi cha kutunzia bastola, simu aina ya nokia, kadi za benki za Kiboko (tano), fomu ya kuweka fedha na faili ndogo lenye nyaraka.
Aliendelea kudai kuwa, pia walikamata faili la TRA, redio ya polisi, hati tatu za kusafiria, unga mweupe ndani ya kikopo angavu cha plastiki, vikopo viwili vyenye unga, chenga chenga za unga ndani ya nailoni nyepesi, hati ya kusafiria ya mshtakiwa Pilly, kadi ya gari Land Cruiser Prado, kadi ya gari Toyota Hilux, kadi ya gari Prado, gari Prado, gari Toyota Hilux, Landcruser Prado na kitabu cha silaha.
Katika kesi hiyo ya kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 251.25 aina ya Heroin inayomkabili mfanyabiashara Ayubu Kiboko na mke wake Pilly Mohammed amedaiwa kuwa katika hati ya ukamataji walikamata vitu mbalimbali ikiwemo bastola moja na risasi saba.
Aidha shahidi huyo alidai kuwa, aliweka alama katika vielelezo hasa vile vilivyodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya, na kisha wakaelekea ofisini kwa hatua zingine ambapo waliwasiliana na mtunza vielelezo SSP Neema na kumkabidhi kama vilivyoorodheshwa kwenye hati ya ukamataji, ambapo vielelezo ambavyo havihusiani na dawa vilibaki chini yake, na magari yalitolewa kama kielelezo yalipokelewa.
Kwa upande wa Wakili wa washtakiwa hao, Majura Magafu alimuhoji shahidi akimtaka aeleze ndani ya nyumba walikuta watu wa ngapi, shahidi akadai walikuta watu wawili ambao ni washtakiwa.
Alipoulizwa kama aliwakuta mabinti wengine, na alidai kuwa hajui umri wao na hawakuwahoji na pia hawakumuona mlinzi, ambapo mashahidi walioshuhudia ni majirani wa washtakiwa.
Shahidi huyo alidai kuwa kielelezo namba 17 (unga mweupe) alikukuta katika choo cha chumbani na alipoulizwa kama kilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali alidai kuwa hajui.
Pia, alidai kielelezo namba 16 walikuta chooni, namba 21 (hatia ya kusafiria) walikuta sakafu ya chini anakolala binti, walichukua kielelezo hicho, ambapo hakuwahoji mabinti kwa sababu baba mwenye nyumba alidai hauhusiki.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 29/2018, Kiboko na mkewe wanadaiwa, Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kuÄşevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 251.25.
No comments: