SERIKALI YASEMA MABADILIKO KATIKA SEKTA YA AFYA HULETA MAENDELEO
MKURUGENZI wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Ntuli Kapologwe amesema changamoto za afya zinazowasilishwa katika mikutano mbalimbali zinalenga kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya afya nchini.
Akiongea leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 7 wa Afya – Tanzania Health Summit uliofanyika Jijini Dodoma Dkt Kapologwe amesema zipo changamoto nyingi katika Sekta ya afya, hivyo ushirikiano wa pamoja utasaidia kutatua changamoto hizo na kuleta mabadiliko kwa jamii.
Dkt Kapologwe ameendelea kufafanua kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI itahakikisha inayaingiza maelekezo yatakayotolewa kwenye Mkutano huo katika mipango ya Hospitali za Halmashauri, Mikoa, Hospitali za Kanda na Taifa ili yaweze kutekelezwa kuanzia ngazi ya msingi.
Aidha ameahidi kuwa katika Mkutano wa waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri ataingiza changamoto zilizotolewa katika Mkutano huo kwa kuwa wao ni watendaji wakuu katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya kwa jamii
Wakati huohuo rais wa Kongamano la Afya Tanzania Health Summit, Dkt. Omary Chillo amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili uchumi wa kati unavyoendana na Nyanja ya Afya nchini.
Dkt. Chilo amesema kuwa washiriki ni tasisi zisizo za kiserikali ambazo zinatoa mada na kujadili jinsi gani wataweza kuboresha afya ya jamii kwa wananchi.
Hata hivyo, ameeleza kuwa katika Mkutano huo watatoa mrejesho wa mikutano mingine iliyowahi kufanyika na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike katika kuboresha Sekta ya afya katika kipindi hiki cha uchumi wa kati.
No comments: