Serikali Kuboresha Maslahi ya Wafanyakazi Inbox
Jonas Kamaleki, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wetu wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akizindua Bunge la 12 ambalo ameahidi kushirikiana nalo kwa karibu.
“Tutaendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wetu wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania, kwa hiyo, watumishi wasiwe na wasiwasi”, alisema Rais Magufuli.
Kuhusu utawala bora katika miaka mitano ijayo, Rais Magufuli ameahidi kuendelea kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma pamoja na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha Tanzania kushika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa, kwa mujibu wa Transparency International; na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa Utafiti Jukwaa la Dunia (World Economic Forum) wa mwaka 2019.
Bunge la 12 lililozinduliwa leo Novemba 13 na Rais Magufuli, limeahirishwa hadi Februari 2, 2021 saa tatu asubuhi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
No comments: