SANGA ATOA SIKU 60 KWA MAMLAKA YA MAJI SONGEA KUKAMILISHA MRADI
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akimtua ndoo ya maji mmoja wa akina mama wa kijiji cha Litisha wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa miradi ya maji Songea. Katikati ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa tenki la maji kijiji cha Nakahuga, Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa tatu kushoto) ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa akiwasilisha tarifa ya mradi wa maji wa Peramiho kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama (kulia) wakati za ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji kwenye Halmashauri ya Songea.
……………………………………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa Siku 60 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa kijiji cha Litisha katika Halmashauri ya wilaya ya Songea.
Mhandisi Sanga ameelekeza hayo Novemba 28, 2020 wakati wa ziara yake ya kukagua na kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa wilayani humo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama.
Akiwa kwenye mradi wa maji wa Litisha unaotekelezwa na wataalam wa ndani kutoka SOUWASA, Mhandisi Sanga alijionea hali halisi ya ujenzi wake ambapo alisema amefarijika kuona kisima kilichochimbwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa kijiji hicho kikitoa maji mengi.
Hata hivyo alisisitiza ukamilishwe haraka na huku akikumbushia dhamira ya Serikali ya kuwasogezea huduma ya maji wananchi wakehasa wanyonge ili kuwapunguzia usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuatilia huduma ya magi.
“Nimefurahi kuonakisima kinatoa maji mengi sana na tenki tayari limekamilika lakini bado miundombinu ya kuwafikishia wananchi maji haijakamilika; maelekezo yangu ni kuwa, ndani ya siku 60 mradi huu uwe umekamilika na wananchi wawe wamepata huduma ya maji,” alielekeza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga aliwahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali haitowaangusha, itahakikisha huduma ya majisafi na salama inawafikia wananchi mapema iwezekanavyo kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
“Ninawahakikishia Serikali mliyoichagua kwa kura nyingi haitowaangusha, iliahidi na sasa inatekeleza, ni suala la muda tu, kero ya maji hapa Litisha na maeneo mengine ya jimbo hili la Peramiho tunakwenda kuimaliza,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alibainisha kwamba kabla ya mwezi huu kumalizika Wizara ya Maji itapeleka kiasi cha shilingi milioni 200 ili kuiwezesha SOUWASA kununua mabomba sambamba na kuhakikisha huduma ya nishati ya umeme imefika kwenye mradi ili wananchi wapate huduma.
“Tutaleta milioni 200 kwa ajili ya kununua mabomba na kujenga miundombinu ya kuwasogezea huduma wananchi wanyonge ili ndani ya siku 60, wawe wamefikishiwa maji,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama kwa jitihada zake za kufuatilia utekelezwaji wa miradi ya maji jimboni humo.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi kwenye halmashauri ya wilaya ya Songea, Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa alisema inatekelezwa kupitia Fedha za Mfuko wa Maji na inahusisha uchimbaji wa visima virefu na ujenzi wa miundombinu ya maji.
Kibasa alisema miradi inatekelezwa kwa awamu mbili tofauti na kwamba awamu ya kwanza inatekelezwa kupitia Mkandarasi Drilling and Dam Construction Agency (DDCA) na inahusisha uchimbaji wa visima virefu 39 katika vijiji 20 vya Halmashauri ya Wilaya ya Songea na kwamba tayari visima 19 vimechimbwa na shughuli inaendelea.
Aidha, aliongeza kuwa awamu ya pili inatekelezwa na wataalam wa ndani na inahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye vijiji nane vilivyothibitika kuwa na maji ya kutosha na kwamba ujenzi umeanza katika vijiji vinne ambavyo ni Litisha, Litowa, Nakahuga na Peramiho B kwa gharama ya shilingi bilioni 2.4.
No comments: