SALMA KIKWETE, LUKUVI, MKUCHIKA WAFUNGUKA, MAJALIWA KUPENDEKEZWA NA RAIS KUWA WAZIRI MKUU

Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa akimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli (Majaliwa akionekana mtulivu na msikivu)

Charles James na Janeth Rafael, Michuzi TV
NI mtu sahihi! Ndiyo kauli ambayo imetolewa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo baada ya jina la Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa kupendekezwa na Rais, Dk John Magufuli kushika nafasi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza ndani ya Bunge, Mbunge wa Isimani William Lukuvi amesema Majaliwa amekua kiongozi makini ambaye amefanya kazi kubwa ya kumsaidia kazi Rais Magufuli lakini pia akiwaongoza mawaziri katika kusimamia majukumu yao.

Amesema kitendo cha Rais Magufuli kulirudisha jina la Majaliwa kwa mara nyingine katika nafasi ya uwaziri mkuu imeonesha jinsi gani yeye anamuamini na ameridhika na utendaji kazi wake kwa miaka mitano iliyopita.

Kwa upande wake Kapteni George Mkuchika amesema Majaliwa amekua kiongozi bora mwenye unyenyekevu na asiyejikweza licha ya nafasi yake kubwa aliyonayo kwani amewasaidia watendaji wengine wa serikali katika kutekeleza majukumu yake.

"Nimpongeze Rais Magufuli kwa kasi kubwa aliyofanya na kumpendekeza Majaliwa kwa mara ya pili ni kielelezo cha namna anavyomuamini katika nafasi ya uwaziri mkuu na sisi tunamuunga mkono kwani hakuna shaka kwamba anaiweza nafasi hii na ameitendea haki." Amesema Mkuchika.

Nae Mbunge wa Mchinga, Mama Salma Kikwete amempongeza Rais Magufuli kwa ushindi mkubwa alioupata na kitendo cha kumpendekeza tena Majaliwa kuwa Waziri Mkuu inaleta tafsiri ya kwamba anamuamini katika nafasi hiyo kubwa na ya kiutendaji ndani ya serikali.

No comments: