NAIBU KATIBU MKUU VIWANDA NA BIASHARA AFANYA ZIARA KWENYE VIWANDA YA KUANGALIA MWENENDO WA BEI YA SARUJI

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Ludovick J. Nduhiye amefanya ufuatiliaji na tathmini katika Viwanda vinavyozalisha saruji, mawakala na wasambazaji nchini, ili kubaini hali halisi ya uzalishaji, usambazaji na mwenendo wa bei ya saruji nchini , kisha kuona ni jinsi gani Viwanda hivyo vimejipanga kukabiliana na changamoto iliyopo ya upatikanaji  na upandaji holela wa bei saruji nchini. Hatua hiyo ni utekelezaji wa Agizo la Mheshimiwa Kassimu Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Viwanda vilivyotembelewa ni pamoja na Kiwanda kinachozalisha Saruji inayotambulika kwa jina la Twiga (Tanzania Portland Cement PLC), Kiwanda cha Saruji cha Lake kinachozalisha saruji ya Nyati vilivyopo Dar es salaam.  Viwanda vingine vilivyotembelewa na ujumbe wa Naibu Katibu Mkuu ni Kiwanda cha Dangote kinachozalisha saruji ya Dangote kilichopo Mtwara na Kiwanda cha Saruji Mbeya kinachozalisha Saruji ya Tembo kilichopo Mbeya.
 
Naibu Katibu Mkuu ambaye aliambatana na maofisa wandamizi toka wizara ya Viwanda na Biashara  alibaini kuwa kati ya viwanda 09 vinavyozalisha saruji nchini kwa sasa, baadhi yake vilisimamisha au kupunguza viwango vya uzalishaji katika kipindi cha mwezi Oktoba na Novemba ili kufanya matengenezo ya mitambo ya uzalishaji Clinker na Saruji.
 
Baadhi ya Viwanda hivyo vilivyokuwa katika vipindi vya matengezo ya kawaida ya kila mwaka na au kufanya uhuishaji wa mifumo ya uendeshaji na uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji nishati ni pamoja na Kiwanda cha Dangote, kiwanda cha Saruji Mbeya na Kiwanda cha  Saruji cha  Portland Tanzania. Hata hivyo, sambamba na matengezo hayo baadhi ya viwanda viliendelea na uzalishaji na usambazaji japo kwa kiwango cha chini kidogo. Kwa sasa Viwanda vyote tayari vimekamilisha ukarabati huo na vimejipanga kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.
 
Aidha Naibu Katibu Mkuu akiwa Dar es salaam alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Paulo Mshimo Makanza Ofisini kwake. Katibu Tawala huyo alisema kuwa bei ya saruji katika mkoa wa Dar es salaam ilipanda kutoka TZS14500 hadi takribani TZS 19000 ya awali kwa  mfuko wa kilogramu 50 na kwa sasa bei ya mfuko wa saruji inauzwa kati ya TZS 14,500 hadi zaidi ya TZS 15,500.
 
Akiongea na Naibu Katibu Mkuu wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Saruji cha Portland Tanzania Bw.  Alfonso Velez alisema Kiwanda chake kinachozalisha saruji  kwa jina la Twiga kimeendelea na uzalishaji wa saruji na kuisambaza kwa wateja wake kwa bei ile ile ya  TZS 13,500 kwa mfuko wa saruji aina 32.5R na TZS 13,800 kwa saruji aina ya 42.5R
 
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kinao uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 160,000 kwa mwezi na takribani tani milioni 2.0 kwa mwaka.  Kiwanda hicho pia kimekuwa kikizalisha clinker ambayo huchukua asilimia 65 hadi 85 ya saruji na kununua ziada ya clinker kutoka Kampuni ya Dangote, Maweni limestone na nchi za nje ili kukidhi mahitaji yake ya ndani ya uzalishaji Saruji. Aidha kiwanda hicho kimejipanga kuongeza uzalishaji  ili kukidhi  ongezeko la mahitaji ya  saruji  linalosababishwa  na ujenzi wa miradi mikubwa  inayohitaji saruji kwa wingi pamoja na ongezeko la mahitaji ya watu binafsi.  
 
Baadhi ya miradi iliyotajwa kuongeza mahitaji ya saruji nchini  na ambayo Viwanda takribani yote yanasambaza saruji ni pamoja na ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Mto Rufiji wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP), ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa Daraja la New Salender Dar es Salaam, Mradi wa ujenzi wa Barabara za Juu Ubungo, ujenzi wa Barabara za Mwendokasi awamu ya pili,  ujenzi wa Barabara zingine za mikoani, ujenzi  wa viwanja vya ndege, uendelezaji wa makao makuu  Dodoma na mahitaji ya watu binafsi ya ujenzi.
 
Akiongea na Naibu Katibu Mkuu wakati wa ziara yake jijini Dar es salaam, Wakala wa Saruji kutoka Kiwanda cha Saruji ya Portland Tanzania,  Dipak Manilal Lal alisema mahitaji ya saruji yemeongezeka nchini na kuwa yeye anauza saruji yote anayoipata kwa siku kwa wateja wake. Na kwa wakati huu hulazimika kila mteja wake apate mifuko 100 ya saruji ili kuhakikisha wote waliofika dukani kwake wanapata saruji. Aidha, Mawakala wengine waliotembelewa jijini Dar es salaamu walikiri kupokea saruji na kuiuza moja kwa moja kwa wateja wao tofauti na zamani ambapo waliweza kuhifadhi saruji inayobaki.
 
Naye Mkuu wa Idara ya Mikakati ya Kibiashara wa Kiwanda cha Saruji ya Lake, IPN Pathall akitoa maelezo yake kuhusu upandaji bei na uhaba wa saruji nchini  kwa Naibu Katibu Mkuu alisema kuwa  uhaba wa saruji nchini ni dalili nzuri ya maendeleo ya kiuchumi unaosababishwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya saruji  kuliko uzalishaji (demand and supply gap) linalotoa changamoto kwa viwanda vinavyozalisha saruji  kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.
 
IPN pia alisema kuwa kiwanda chake kinachozalisha Saruji inayoitwa Nyati hakikusitisha uzalishaji na wala hakikupandisha bei ya saruji bali kimeendelea na uzalishaji ili kuendana na mahitaji yanayokuwa kila siku ya wateja wake pamoja na miradi mikubwa. Aidha bei ya mfuko wa saruji imeendelea kuuzwa kwa TZS 12,710 kwa saruji aina ya 32.5R na TZS 13500 kwa saruji aina ya 42.5R.
 
Naye Mtendaji Mkuu wa Uzalishaji wa Kiwanda cha Saruji ya Lake Biswajeet Mallik amesema kiwanda cha Lake kimeendelea na uzalishaji ambapo kwa sasa kinazalisha tani 50,000 kwa mwezi na tani 600,000 kwa mwaka na kinajipanga kuongeza uzalishaji huo ili kukidhi mahitaji ya soko linalokua kila siku. Kiwanda hicho pia kimekuwa kikizalisha Clinker kwa ajili ya mahitaji yake na kununua nyingine kutoka   kiwanda cha Dangote na Maweni Limestone.
 
Aidha akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wakati wa ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Alphayo Kidata alisema kuwa bei ya saruji ilipanda kutoka TZS 13500 hadi TZS 23000.  Aidha alisema bei hiyo kwa sasa imeanza kushuka hadi TZS 14,000 na 15,000 kwa mfuko.
 
Pia katika ziara yake Naibu Katibu Mkuu alikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Rehema Madenge ambaye alieleza kutokana na uhaba huo bei ya saruji katika mkoa wake ilipanda hadi kufikia TZS 24,000 kwa mfuko na sasa imeshuka hadi TZS 15,000.
 
Akitoa maelezo mbele ya Naibu Katibu Mkuu alipotembelea Kiwanda cha Dangote, Mtendaji Mkuu na Meneja wa Kiwanda cha Dangote nchini Tanzania Bw. Abdullahi Baba alisema kiwanda chake kilisimimisha uzalishaji wa saruji tangu mwezi Oktoba 2020 ili kufanya matengenezo ya mitambo yake pamoja na kukamirisha kusimika mitambo ya uzalishaji umeme baada ya kufanya maamuzi ya kimkakati ya kununua mitambo yao wenyewe na kuachana na utaratibu wa kununua nishati hiyo kutoka kampuni nyingine binafsi iliyopewa kandarasi mwaka 2018 ili kuzalisha umeme na kukiuzia kiwanda ambao umekuwa  na changamoto kadhaa na wa gharama zaidi.
 
Meneja huyo amesema mchakato huo wa kuhama kutoka matumizi ya mkandarasi huyo binafsi kwenda utumiaji wa mitambo ya Kampuni nao umechangia katika kuathiri uzalishaji na upatikanaji wa saruji nchini. Pamoja na hayo matengenezo ya mwisho wa Mwaka kwa utaratibu wao huwa yanafanywa kila mwaka mwezi Aprili ambao kwa tathmini yao ni mwezi ulio na mahitaji ya saruji kidogo kutokana na mvua nyingi. Hata hivyo, kwa mwaka huu 2020 matengenezo hayo yamefanyika mwezi Oktoba badala ya Mwezi Aprili kutokana na ukosefu wa vipuri vinavyoagizwa nje ya nchi kutokupatikana kwa sababu ya janga la Corona.
 
Vile vile, Meneja huyo alieleza kuwa katika kipindi hicho Kiwanda kilihuisha mfumo wake wa Tehama unaotumiwa katika shughuli zake za utendaji. Zoezi hilo la uhuishaji wa mfumo pamoja na mambo mengine liliathiri usambazaji wa saruji na hivyo kuchangia upatikanaji  hafifu usiokidhi mahitaji makubwa ya saruji yaliyoongezeka.
 
Meneja huyo alisema kuwa katika kipindi hicho kiwanda hakikupandisha bei na saruji imekuwa ikiuzwa kwa bei ya TZS 11,860 kwa saruji ya 32.5 na TZS 12,110 kwa saruji 42.5 bila VAT. Aidha kiwanda kimejipanga kuhakikisha kinazalisha saruji tani milioni 1.1 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu(2020) na kinalengo la kuongeza uzalishaji ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya saruji nchini.  Kwa ujumla Uongozi wa Kampuni ya Dangote nchini Tanzania umeahidi kuhakikisha unafanya uwekezaji na kuongeza uzalishaji wa saruji ili kukidhi mahitaji ya soko na kutoa mchango stahiki katika mchakato wa maendeleo ya nchi.
 
Naye, Katibu wa Kampuni  na Mshauri wa mambo ya Kisheria wa Kiwanda cha saruji Mbeya, Ian Almachius  alimueleza Naibu Katibu Mkuu kuwa kiwanda hicho kinachozalisha saruji kwa jina la Tembo   kilisimamisha uzalishaji wa saruji kuanzia tarehe 14 hadi 17 Oktoba  2020 kwa ajili ya matengenezo ya kila mwaka. Pamoja na hayo alisema kiwanda hicho kinauweza kuzalisha tani takribani 370,000 kwa mwaka.
 
Ian amesema kuwa kiwanda hakikupandisha bei ya saruji ambapo mfuko umekuwa ukiuzwa   TZS 13700 kwa saruji aina ya 32.5 na TZS 17200 kwa saruji aina ya 42.5. Pia aliongeza kuwa kiwanda hicho huzalisha Clinker kwa ajili ya matumizi yake na hununua clinker kutoka kiwanda cha Dangote na Maweni Limestone ili kukidhi mahitaji yake.
 
Kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto ya umeme na uwezo wake mdogo wa kuzalisha clinker ambayo ni malighafi muhimu na wakati huo kushindwa kupata malighafi hiyo kwa wakati toka kwenye viwanda vinavyowauzia.
 
Aidha Serikali imesisitiza kuhusu umuhimu wa kiwanda hicho kupanua uwezo wake wa kuzalisha clinker ili kuendana na uhitaji wa mitambo iliyosimikwa kuzalisha saruji yenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.1 ili kuongeza ufanisi na tija toka hali ya sasa ya uzalishaji wa asilimia chini ya 40(%) ya uwezo uliosimikwa kwa Mwaka.
 
Akiwa Ruvuma, Naibu Katibu Mkuu alikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Steven Mashauri Ndaki ambaye alimueleza kuwa katika Mkoa wake bei ya saruji ilipanda hadi kufikia TZS 24,000 kwa mfuko na sasa imeanza kushuka na inauzwa kwa TZS 15,000 kwa mfuko.
 
Sambamba ziara ya Naibu Katibu Mkuu; Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara inayoongozwa na Mkurugenzi wa Viwanda Mhandisi Ramson Mwilangali nayo imeendelea na ufuatiliaji na tathmini ya suala hilo katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa.
 
Hadi sasa Timu hiyo imefanikiwa kutembelea Kiwanda cha Saruji cha Tanga kinachozalisha saruji kwa jina la Simba, Kiwanda cha Saruji Kilimanjaro kwa jina la Kilimanjaro, Kiwanda cha Kimataifa ya Jun Yu inayozalisha saruji kwa jina la Moshi, na Kiwanda cha Maweni Limestone kinayozalisha clinker na kuviuzia viwanda vingine vinavyotengeneza saruji. Viwanda vyote vilivyotembelewa vimekiri kutokupandisha bei ya saruji na vimekuwa vikiendelea na uzalishaji na kujipanga kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko linalokua siku hadi siku.
 
Tanzania ina viwanda 13 vya saruji, iwapo vyote vitafanya kazi ipasavyo vinaweza kukidhi mahitaji yote ya saruji nchini ambayo ni takribani tani milioni sita kwa mwaka na kukidhi mahitaji ya miradi mikubwa inayoendelea nchini.
 
Viwanda ambavyo vinazalisha saruji kwa sasa ni takribani viwanda tisa ambavyo ni pamoja na Kiwanda cha Saruji cha Portland Tanzania (Twiga),  Kiwanda cha Dangote Group ( Dangote Mtwara), Kiwanda cha Saruji  ya Lake ( Nyati), Kiwanda cha Saruji Tanga (Simba), Kiwanda cha Saruji Mbeya(Tembo), Kiwanda cha Saruji Kilimanjaro (Kilimanjaro). Viwanda vingine ni pamoja   Kiwanda cha Saruji cha Fortune (Diamond), Kampuni ya Amsons (Camel) na Kampuni ya Maweni Limestone inayozalisha Clinker peke yake.
 
Viwanda ambavyo vilikuwa vinazalisha saruji na kwa sasa vimesimamisha uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali ni pamoja na  Kiwanda ya Xinghao Group ( Lulu) Kampuni ya Saruji Kisarawe (lucky), Kampuni ya Saruji Arusha  na  Kampuni ya  Uchimbaji ya Athi River ( Rhino).
 
Wizara ya Viwanda na Biashara imechukua hatua ya kufanya tathimini ya uzalishaji, usambazaji na bei ya saruji kwa kutembelea viwanda vyote vinavyozalisha saruji nchini baada ya bei kupanda kuanzia kipindi cha mwezi Oktoba 2020 katika mikoa yote nchini.

No comments: