MWENYEKITI WA CCM BWAGAMOYO AREJESHA KIWANJA CHA CHAMA

 Na Mwandishi wetu, Manyara 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Bwagamoyo Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Charles Mbaluka amerejesha kiwanja cha chama hicho alichokuwa amejimilikisha kinyume cha utaratibu tangu mwaka 2015.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu ameyasema hayo Mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Makungu amesema kitendo cha kiongozi huyo kujimilikisha mali ya umma kinatafsiriwa kuwa ni kosa la kutumia madaraka vibaya chini ya kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

Amesema awali TAKUKURU Wilayani Kiteto ilipokea taarifa ikimtuhumu Mbaluka kwa kujimilikisha na kuuza sehemu ya kiwanja cha CCM Kata ya Bwagamoyo kilichotolewa na Serikali ya Kijiji cha Bwagamoyo mwaka 2013 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya CCM kata hiyo.

Amesema uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU Wilayani Kiteto umethibitisha kuwa CCM mwaka 2013 ilipokea kiwanja kwenye mtaa wa Msente chenye ukubwa wa mita 930.776.

"Uchunguzi wetu imebaini kuwa mwaka 2015 Mwenyekiti huyo kwa kuvunja maadili ya umma na chama chake alijimilikisha sehemu ya kiwanja kwa kujengwa nyumba na kuuza sehemu nyingine kwa shilingi 700,000 ya kiwanja hicho." Amesema.

Amesema hata hivyo Mwenyekiti huyo amekiri kujimilikisha kiwanja hicho kinyume cha sheria na kitakabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Patrick Songea kwa siku itakayopangwa ili awakabidhi viongozi wa CCM wa kata ya Bwagamoyo kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa.

"Kwa waliosikiliza na kusoma hotuba ya Rais John Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 katika ukurasa wa 16 wa yake alisisitiza pamoja na kazi kubwa iliyofanyika ya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wala rushwa, wezi na wabadhirifu wa mali ya umma bado wapo." amesema Makungu.

Ametoa rai kwa Baraza la wadhamini wa CCM kuzitambua mali za chama kata zote Mkoani Manyara vikiwemo viwanja na kuhakikisha vinapatiwa hati miliki ili kuepusha mali hizo kuporwa na baadhi ya viongozi wa chama wasio waadilifu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Hole Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.

No comments: