Mwakinyo amchapa kwa TKO Muargentina, kuwania mkanda wa Dunia

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo amemtwanga kwa ‘technical knockout (TKO mpinzani wake Jose Carlos Paz wa Argentina na kufanikiwa kuutetea mkanda wake wa mabara wa uzito wa super welter unaotambuliwa na shirikisho la WBF. 

Mwakinyo alifanikiwa kushinda mkanda huo raundi ya nne baada ya kumshambulia mpinzani wa kwa ngumi nyingi na mwamuzi Edward Marshall aliingilia kati kabla ya kumaliza pambano hilo lililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sport chini ya mkurugenzi wake, Kelvin Twissa. 

Ushindi huo umempa nafasi Mwakinyo kuwania mkanda wa dunia wa WBF dhidi ya bondia Lasha Gurguliani wa Georgia ndani ya miezi mitatu kwa miezi mitatu kuanzia sasa kwa mujibu wa rais wa WBF Howard Goldberg. 

Akizungumza mara baada ya kushinda pambano hilo, Mwakinyo alisema kuwa ushindi huo ni wa Tanzania nzima ambao waliamua kumpa sapoti katika pambano hilo na mengine yaliopita. 

“Haikuwa kazi rahisi kushinda, Paz ni bondia mzuri, kama nilivyosema, nafanya mazoezi kutokana na ubora wa mabondia ninao pambana nao. Namshukuru Mungu kuniwezesha kushinda katika pambano hili,” alisema Mwakinyo. 

Paz alikubali kushindwa kihalali katika pambano hilo na huku akimpa sifa kubwa Mwakinyo kuwa ni bondia mzuri. Mkurugenzi wa Jackson Group Sport, Kelvin Twissa aliwapongeza mashabiki wa ngumi waliofika katika pambano lao la kwanza la ngumi za kulipwa nchini. 

Twissa alisema kuwa pambano hilo limefungua njia ya kuandaa mapambano mengine mengi yenye hadhi ya kimataifa na yenye ubora wa hali ya juu. 

Katika pambano linguine, bondia Fatuma Zarika wa Kenya alifanikiwa kutwaa ubingwa wa WBF baada ya kushinda kwa pointi ya mpinzani wake Patience Mastara wa Zimbabwe. 

Zarika alishinda kwa pointi 97-93 kutoka kwa jaji Anthony Rutta ambapo Jaji Pendo Njau alimpa Zarika 98-92 na jaji alitoa pointi 98-92. 

Pia bondia Zulfa Macho ameanza vyema katika ngumi za kulipwa baada ya kushinda kwa pointi dhidi ya Alice Mbwewe wa Zambia. 

Zulfa alishinda kwa pointi 59-56 kutoka kwa jaji John Chagu, 58-56 (Ibrahim Kamwe) na 59-55 kutoka kwa jaji Anthon Rutta. 

Pia bondia Hussein Itaba alitoka sare dhidi ya bondia Alex Kabangu katika pambano ambao matokeo yake yalikuwa na utata mkubwa. 

Utata huo ulitokana na matokeo kumtangaza kuwa Kabangu ameshinda pambano hilo, jambo ambalo lilimfanya Itaba kugoma kutoka ulingoni akigomea matokeo hayo pambano hilo, Jaji Ali "Champion" Bakari na Ibrahim Kamwe walitoa sare ya pointi 94-94 kila mmoja huku refa na jaji mkongwe nchini John Chagu alitoa ushindi kwa Kabangu kwa pointi 94-95. 

Kaimu rais wa kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) Aga Peter alitatua utata huo na kupanda ulingoni na kubadili matokeo hayo katika pambano ambalo lilikuwa na upinzani mkubwa huku kila bondia akianguka mara moja katika raundi tofauti.
Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa akimpongeza bondia Hassan Mwakinyo mara baada ya kutetea vyema ubingwa wa mabara wa uzito wa super welter unaotambuliwa na shiriksiho la WBF. Mwakinyo alishinda kwa TKO raundi ya nne.
Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa (nyuma) akimvisha mkanda bondia Hassan Mwakinyo mara baada ya kutetea vyema ubingwa wa mabara wa uzito wa super welter unaotambuliwa na shiriksiho la WBF. Mwakinyo alishinda kwa TKO raundi ya nne.
mabondia Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wakipambana

No comments: