MCHIMBAJI MDOGO WA MADINI AINA YA RUBY AIBUKA BILIONEA BAADA YA KUPATA MADINI YENYE THAMANI YA BILIONI 1.7/=

 

Na Woinde Shizza, Michuzi Tv Arusha

 

Mchimbaji mdogo mdogo wa Madini ya Ruby yaliyopo katika kata ya Mundarara wilayani Longido Mkoani Arusha Sendeu Laizer ameibuka kuwa tajiri katika sekta hiyo baada kupata tani tano za madini hayo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.7.

 

Hiyo ni mara ya pili kwa wachimbaji wadogo wadogo kupata utajiri kwani mchimbani mwingine alikuwa Sanniu Laizer aliyefanikiwa kupata madini ya Tanzanite yenye thamani ya zaidi ya bilioni 8.

 

Akizungumza na wataalam na watendaji wa sekta ya madini waliotembelea mgodi huo mmiliki wa mgodi huo Gabriel sendeu  Laizer amesema mafanikio hayo ni matokeo ya hatua zinazochukuliwa na serikali kuwajengea wachimbaji wadogo mazingira mazuri ya uchimbaji.

 

Laizer ni kijana wa pili kutoka jamii ya wafugaji wa kimasai kuibuka Bilionea kupitia madini katika kipindi cha kifupi wa kwanza akiwa ni kijana mwingine Saniniu  Laser ambaye alipata kilo zaidi ya 11 za madini ya Tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Bilion 8.

 

Alisema na kuishukuru sekta ya madini hususani Rais Dr. John  Magufuli kwa kuwathamini wachimbaji wadogo na kuwatetea  hatua ambayo ndio iliyochangia mafanikio yake kwa sasa na sio vinginevyo.

 

Pia amewashauri wachimbaji wenzake wadogo wa madini kuendelea kuchimba bila kukata tamaa kwani kazi hiyo inahitaji uvumilivu  na kujitoa kwa dhati.

 

Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini hayo wamesema kupatikana kwa kiasi hicho kikubwa cha madini kimewaongezea ari ya kuendelea kuchimba japo wanasema wanakabiliwa na tatizo la mitaji na vitendea kazi ,

 

Mmoja wa wachimbaji wadogo katika eneo hilo Michael  Lekule  Laizer ambaye alikuwa mbunge mstaafu wa Jimbo la Longido na Mwenyekiti  Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi{CCM} amesema  upo uwezekano wa kunufaika na rasilimali hiyo kama taasisI za fedha zitaona umhimu wa kuwasaidia kwa kuwapa mikopo ya muda mrefu.

 

Viongozi wa vyama vya wachimbaji wa madini mkoa wa Arusha akiwemo Alfred Antony ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wachimbaji na Jeremia Simion ambaye ni mwenyekiti wa wachimbaji wa kati wamesema wachimbaji wote wadogo wana ari ya kuchimba na wanafurahia mazingira waliyowekewa.

 

Naye Mkuu wa wilaya ya Longido ,Frank Mwaisumbe amewataka wachimbaji wadogo kuona umuhimu wa kuuunganisha nguvu pamoja ili waweze kupata vitendeakazi vya kuwawezesha kuchimba kisasa zaidi na kunufaika na rasilimali za madini ambayo sasa yame wekewa utaratibu mzuri wa kuhakikisha yanawanufaisha wazawa.

 

Aidha mwaisumbe pia amewashauri wachimbaji wadogo kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ukiwemo kudhibiti utoroshaji wa madini ili yaendeleee kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla .

 

Mtaalam wa kutoka wizara ya  madini ambaye ni mjiolojia mwandamizi Mussa Shanyange amesema madini ya Ruby  ni miongoni mwa madini yenye thamani kubwa ambayo yanapatikana kwa wingi katika eneo hilo 

 

Kwa upande wake Kamishna wa Madini wa Mkoa wa Arusha (RMO),Aidan Muhando amempongeza Sendeu  Laizer kwa kuona umuhimu wa kufanya uchimbaji kwa uwazi na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa hatua ambayo imemuwezesha kupata mafanikio yeye mwenyewe , serikali na jamii kwa ujumla.

 

Hata hivyo amewataka wachimbaji wengine wenye leseni za kuchimba  katika maeneo hayo ambao hawajaanza kuhakikisha wanaanza kuchimba ili kuongeza uzalishaji .

 

Amesema baadhi ya wachimbaji wamepewa leseni lakini hawachimbi utaratibu ambao haukubali na kama hatua hiyo itaendelea watalazimika kuchukua hatua ya kuyachukua maeneo hayo na kuwapa watu wengine wenye uwezo wa kuchimba 

 

Wananchi wa Kijiji cha Mundarara wamesema hatua ya kupatikana kwa bilionea  katika Kijiji chao imewapa matumaini makubwa ya kuanza kupata ufumbuzi wa matatizo mengi yanayowakabili 

 

Kwa mujibu wa kamishina  Madini ya Ruby pamoja na kupatikana katika wilaya hiyo ya Longido Mkoa wa Arusha pia yanapatikana wilaya za mkoa wa Tanga , na wilaya za mkoa  Dodoma 



No comments: