MAHAKAMA IMEWAHUKUMU WATU WAWILI KULIPA SH. MILIONI 1.5 KILA MMOJA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu Mhandisi Baraka Mtunga (43) na Rajabu Katunda (42) kulipa faina ya Sh. Milioni 1.5 kwa kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza huduma ya intaneti bila kibali na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 200.

Aidha washtakiwa hao, wametakiwa kulipa fidia ya Sh. 267.656.794.30 baada ya kuingia makubaliano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kufuatia kukiri makosa  yao.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameshalipa Sh. Milioni 200 kati ya fedha hizo walizokubaliana kulipa ambapo kiasi cha Sh 67,659.794.30 kilichobaki wanapaswa kulipa ndani ya miezi sita kama makubaliano yao yanavyosema.

Hukumu hiyo imesomwa leo Novemba 24,2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele baada ya kuwasomea washtakiwa makubaliano baina yao na DPP na kukiri makosa mawili ya kutumia mitandao kilaghai na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), hasara ya zaidi ya sh. Milioni 260.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Matembele amesema Mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili, na makubaliano yaliyoingiwa kati ya washtakiwa na DPP.

Kabla ya kusomwa kwa adhabu ya mahakama, Hakimu Matembele aliuliza  upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ndipo wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon alipoomba itolewe adhabu kali kwa washtakiwa kwa sababu suala la  mawasiliano ni suala nyeti na pia hatari kwa Taifa.

Upande wa utetezi waliomba  kupunguziwa adhabu ukizingatia wameonesha busara ya kukiri makosa yao hivyo aliomba mahakama itoe adhabu ya faini ndogo kutokana na ushirikiano wa washtakiwa waliyouonesha wa kukiri kosa na pia ni vijana ambao wanafamilia na watoto wanawategemea, kwa a naomba adhabu ambayo itawafanya wafanye shughuli zao na kuweza kulipa deni lililobaki.

Akisoma adhabu Hakimu Matembele amesema katika shtaka la kwanza kila mshtakiwa atalipa Sh.milioni moja na akishindwa atatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani huku katika shtaka la pili kila mmoja anapaswa kulipa faini ya Sh 500,000 ama akishindwa basi ataenda jela miaka miwili, adhabu nitaenda sambamba.

Hata hivyo, Hakimu Matembele ametupilia mbali ombi la  upande wa utetezi kupitia Wakili wao Hajra Mungula aliyeomba washtakiwa warudishiwe simu zao za mkoni mbili  na kompyuta mpakato moja (laptop) kwa sababu hazikuwepo kwenye makubaliano ya DPP na pia havikuwa sehemu ya kesi hiyo.

"Akijibu ombi hilo, Hakimu Matembele amesema, mahakama imejiuliza swali kuwa ni kwanini vitu hivyo vilipelekwa mahakamani ?haiwezekani kwamba vifaa hivi havikutumika katika utendaji wa kosa na kama ulikuwa hutaki, ulitakiwa kupinga visitolewe mahakamani kama kielelezo, kwa hiyo natupilia mbali maombi hayo na vifaa hivi vinataifishwa kuwa mali ya Serikali," alisema Matembele.

Mapema ilidaiwa kati ya Desemba 13, 2019 hadi Septemba 28 2020, katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo kijijiji cha Kanjoo, Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani na maeneo mbali ya jiji la Dar es Salaam,  washtakiwa waliisababishia TCRA hasara ya sh 267,656,794.30.

Katika shtaka la pili, washitakiwa hao wanadaiwa kutumia mitandao kwa njia za kilaghai, wakiwa na nia ya kukwepa malipo halali ya kodi, walisambaza huduma hiyo ya internet. 

No comments: