KUMEKUWEPO NA ONGEZEKO KUBWA LA WAZAZI WANAOWALETA WATOTO WAO KLINIKI KUPATA CHANJO YA MAGONJWA MBALIMBALI

Na PATRICIA KIMELEMETA

CHANJO kwa mtoto mchanga ni muhimu ili kuhakikisha inalinda na magonjwa mbalimbali mara baada ya kuzaliwa, lakini pia inasaidia mtoto kupata malezi na makuzi bora na kumuepusha na maradhi yanayoweza kuhatarisha maisha au ukuaji wake.

Chanjo huokoa maisha ya watoto milioni 3 kila mwaka Duniani kote kwa sababu hukinga maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Mganga wa Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, Dk Lucy Mpayo amesema kuwa, ssa hivi kumekua na ongezeko kubwa la wazazi wanaowaleta watoto wao kliniki kwa ajili ya kupata chanjo ya magonjwa mbalimbali tofauti na hapo awali.

Amesema kuwa, ongezeko hilo limetokana na elimu inayotolewa na serikali ya kuwahamasisha wazazi na walezi kufika kwenye vituo vya afya vilivyopo karibu na makazi yao ili kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo.

"Awali, wazazi na walezi walikua hawawapeleki watoto kupata chanjo ya kuwakinga na magonjwa mbalimbali, lakini sasa hivi kumekua na ongezeko kubwa la wazazi kufika vituo vya afy vilivyopo karibu na maeneo yao ili kuhakikisha watoto wanapata chanjo," amesema Dk.Mpayo.

Ameongeza kuwa, hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa vituo vya afya kila kata na serikali kuendelea kutoa elimu ya chanjo pamoja na kuwaelimisha wazazi au walezi umuhimu wa watoto wao kupata chanjo.

Amesema kutokana na hali hiyo, matokeo chanya yameweza kuonekana baada ya kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa wazazi au walezi kufika kwenye vituo hivyo na kupata elimu ya malezi, makuzi na changamoto zinazoweza kuwakuta watoto walio chini ya miaka minane,jambo ambalo linasaidia kupunguza magonjwa kwa watoto.

Amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ili ongezeko hill liwe kuwa, jambo ambalo litarahisisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Kisayansi chanjo ni kitendo cha kupewa kinga mwili kwa njia ya kuamsha vitoa kinga viwe tayari kupambana na adui ambaye wanamjua tayari.

Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo.

No comments: