KILA KONA YAJA NA SULUHISHO LA ULINZI WA WATOTO MASHULENI


Meneja mauzo wa Kila Kona Ltd  Saimon Mahundi akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na umuhimu wa programu ya Ulinzi wa mtoto wakati wa semina maalumu iliyowakutanisha na wadau mbalimbali wa elimu kuhusiana umuhimu wa teknolojia katika sekta ya elimu, leo jijini Dar es Salaam.
Mafunzo yakiendelea.
Mkuu wa shule ya AL IRSHAAD Zena Kazukamwe akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na umuhimu wa teknolojia katika ya elimu na kuzishauri shule kufuata mfumo huo, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kila Kona (Ltd) Salim Rajab akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo maalumu kuhusiana na mchango wa teknolojia katika sekta ya elimu na ameeleza kuwa wataendelea kutoa huduma katika kuhakikisha taifa haliachwi nyuma katika teknolojia hasa katika sekta ya elimu, leo jijini Dar es Salaam.


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

KUTOKANA na visa vya watoto kupotea wakiwa wanakwenda shuleni na kurejea majumbani kampuni ya Kila Kona (Ltd) imekuja na suluhisho maalumu la kukomesha matukio hayo ambapo kupitia kadi maalumu mzazi ataweza kupata taarifa za mtoto kuanzia anapotoka nyumbani, akiwasili shuleni na anaporejea nyumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa semina maalumu kwa walimu wa shule mbalimbali za awali na msingi kuhusiana na mchango wa teknolojia katika sekta ya elimu, Meneja mauzo kutoka kampuni ya  Kila Kona, Saimon Mahundi amesema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la upotevu wa watoto hasa wakiwa wanakwenda shuleni na kurejea majumbani.

"Kila Kona inajali usalama  wa watoto katika kuhakikisha wanatimiza malengo yao, hivyo katika kuhakikisha watoto wanakua salama kupitia programu maalumu mzazi atapata ujumbe kupitia simu yake ya mkononi tangu mtoto akipanda basi la shule, akiwasili shuleni na atakapokuwa anarudi nyumbani na hii ni kupitia kadi maalumu atakayokuwa nayo mtoto."Amesema.

Amesema kuwa kupitia programu hiyo mzazi pia atapata kujua mahudhurio ya mtoto kila siku na huduma hiyo inapatikana Kila Kona kwa gharama nafuu. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kila Kona (Ltd) Salim Rajab amesema, lengo ni kukutana na wadau hao wa elimu ni kuzungumza juu ya teknolojia katika sekta ya elimu.

"Dunia imehama na kwa sasa teknolojia ni nyenzo katika kila sehemu, na kutokana na umuhimu wake tumeamua Kupambana katika kuhakikisha Tanzania na Afrika kwa ujumla hatuachwi nyuma katika teknolojia hasa katika sekta ya elimu." Ameeleza.

Amesema kuwa Kila Kona imekuwa ikifanya kazi na shule zipatazo tano na kupitia ''Kila Kona School App" walimu, wanafunzi kwa kushirikiana na wazazi wanaweza kujifunza masomo mbalimbali kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya AL IRSHAAD iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam Zena Kazukamwe amesema, wakiwa wadau wa elimu wamepokea vizuri programu kutoka Kila Kona na imetoa matunda bora hasa katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona.

"Licha ya Kupambana na changamoto wakati wa janga la Corona lakini tulifanikiwa vizuri tuliweza kufundisha na kutoa mitihani kwa mtandao, ni vyema shule zikajiunga na mfumo huu ili kuendelea kuijenga sekta ya elimu." Amesema.

Kila Kona ni kampuni yenye mlengo wa kuimarisha sekta ya elimu (awali, msingi na Sekondari) kupitia teknolojia inayokua siku hadi siku ambapo kupitia Kila Kona School App wanafunzi, walimu kwa kushirikiana  na wazazi watapata rasilimali zitakazowasaidia katika masomo yao.

No comments: