KAMALA HARRIS, MAKAMU WA RAIS NA MWANAMKE MWEUSI WA KWANZA NCHINI MAREKANI

Na Leandra Gabriel,  Michuzi TV

MSHINDI wa kiti cha Urais nchini Marekani amepatikana, Joe Biden (77) na Kamala Harris (56) wamemwondoa madarakani Donald Trump (74) kutoka chama cha Republican, aliyeongoza kwa msimu mmoja pekee.

Kamala Harris mwanamke mweusi mwenye asili ya India anakuwa mgombea mwanamke wa tatu kugombea nafasi hiyo ya juu nchini humo akitanguliwa na Geraldine Ferraro (1984,) na Sarah Palin (2008.)

Kamala binti wa wahamiaji kutoka Jamaica na India alizaliwa Oktoba 24, 1964 huko Oakland, California akipewa jina la Kamala Devi Harris kutoka kwa baba Donald Harris Profesa wa masuala ya uchumi na mama Shyamala Gopalan Harris aliyekua mwanabaiolojia na mtafiti wa magonjwa ya saratani hasa matiti.

Kamala alipata elimu ya awali katika shule za Umma ambazo asilimia 95 ya wanafunzi walikuwa raia wa Amerika na baadaye watoto wenye asili ya Afrika walifikia asilimia 40.

Mwaka 1986 Harris alimaliza shahada ya awali ya masuala ya siasa na uchumi katika chuo cha Howard na kurejea California kusoma shule ya sheria katika chuo kikuu cha California.

Kamala aliyekuwa Seneta wa California na kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo kwa miaka 20 amewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo uwakili katika ukanda wa San Francisco na baadaye kuongoza idara ya sheria.

Januari 21, 2019 alitangaza kuwania nafasi ya Urais kupitia video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na baadaye kutokea katika kituo cha ABC's katika "Good Morning America."

Agosti 11 mwaka huu Biden alimtangaza Harris kuwa mgombea mwenza wa kiti cha Urais kupitia Chama cha Democratic na kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kutoka kusini mwa Asia kuwania nafasi hiyo.

Licha kuzaliwa, kukua, kusoma na kuabudu katika jamii za kiafrika pia ana historia ya kubaguliwa hali iliyomsukuma kuwa mtetezi wa wazi wa haki za wahamiaji na wanawake, na masaa machache kabla ya Biden kutangaza kuwa mgombea mwenza wa kiti cha Urais, kupitia ukurasa wake wa Twitter Kamala alichapisha;

"Wanawake weusi na wengineo wasio weusi kwa siku nyingi wamekuwa wa uwakilishi wa chini kati ya wanaochaguliwa na Novemba tuna nafasi ya kubadilisha hilo." Aliandika Kamala.

Kamala ameolewa na Douglas Emhoff mwaka 2014 hadi sasa.


 

No comments: