Hatutakwenda Kupiga Makofi – SANGA
Mbunge mteule wa Makete (CCM), Mhe. Festo Richard Sanga amesema wabunge wateule wanaotokana na CCM hawatakwenda kupiga makofi na badala yake watakosoa kistaarabu.
Mhe. Sanga ameyasema hayo leo alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hii leo katika viwanja vya Bunge mara baada ya kujisajili bungeni humo akijibu tuhuma zinazotolewa na baadhi ya wapinzani kwamba eti Bunge la 12 halitakosoa kwa sababu wabunge wengi wanatokana na Chama Tawala.
“Hatutakwenda kupiga makofi, kauli mbiu ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli inasema ‘Hapa Kazi Tu’, hii ni Serikali ya kazi, waziri asiyefanya kazi hatutampigia makofi, tutapaza sauti kuliko wale waliokua wakipinga miradi ya maendeleo”, alisema Sanga
Naye mbunge mteule wa viti maalum (CCM) Mkoa wa Kagera, Mhe. Neema Lugangira amewataka wapinzani waheshimu maamuzi ya wananchi.
“Tuheshimu maamuzi ya wananchi, dhana ya kusema Bunge hili halitakosoa ni dhana inayolenga kutudhoofisha, nitakosoa, ni jukumu langu kuwasemea wanawake na mashirika yasiyo ya Serikali kwa sababu ndio walionituma”, alisema Lugangira.
Kwa upande wake, mbunge mteule wa Malinyi (CCM), Mhe. Antipas Mgungusi amesema Bunge la 12 halitakuwa na matusi kama ilivyozoeleka na kwamba hawatasusia mijadala yenye maslahi kwa Taifa.
“Hatuwezi kunyamaza kama watu wanavyodhani, tutakosoa, tutashauri na kupongeza pale itakapohitajika, hakutakuwa na matusi kama tulivyozoea”, alisema Mgungusi
Pamoja na hayo, mbunge mteule wa Morogoro Mashariki (CCM)( weka jina lake) amesema wabunge waliochaguliwa wanakwenda kukosoa kwa lengo la kujenga.
No comments: