CDF, JAMII FORUMS WAINGIA MAKUBALIANO KUPINGA UKATILI DHIDI YA WATOTO, WANAWAKE
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti (wa kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Kiraia ya Jamii Forums, Mexence Melo (wa kulia) wakionyesha mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika kupaza sauti kwa jamii katika masuala ambayo yanaathiri Watoto, Wanawake na kupinga ukatili dhidi yao kwa kipindi cha miezi mitatu.
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
SHIRIKA la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Jamii Forums zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika kupaza sauti kwa jamii katika masuala ambayo yanaathiri Watoto, Wanawake na kupinga ukatili dhidi yao kwa kipindi cha miezi mitatu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti amesema wameona kuna umuhimu wa kuwa na ushirikiano huo kutokana na Jamii Forums kufikiwa na wasomaji wengi katika Jamii, ambayo itasiadia kukuza uelewa kwa Jamii hizo kuhusu haki za Watoto na Wanawake.
Koshuma amesema ushirikiano huo ni muhimu na utapaza sauti kwa jamii kutokana na kukithiri kwa matukio hayo ya ukatili wa Watoto, Watoto wa Kike na Wanawake yakiweno matukio ya Ubakaji na Vipigo.
Pia ametoa Mfano visa vya Mimba za Utotoni zilizoongezeka kutoka asilimia 23 hadi kufikia asilimia 27 ikilinganishwa kwa idadi ya Watoto wapatao 27 wanapata Ujauzito kati ya Watoto 100 nchini.
“Suala la Rushwa ya Ngono, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetoa Ripoti yake inayoonyesha kukithiri kwa Ngono, Vyuoni kwa zaidi ya asilimia 84 kwa Wanawake, na asilimia 15 pekee Wanaume wanaathirika na Rushwa hiyo, ambayo baadae itawaletea madhara kwa Jamii yao.” amesema Koshuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums, Mexence Melo amesema wataisaidia CDF kupaza sauti kwa jamii kupinga matukio ya ukatili wa Watoto na Wanawake, Melo amesema tayari Taasisi hizo zimejengeana uwezo kwa Watendaji wake kuelewa zaidi masuala hayo ya ukatili na matukio ya unyanyasaji.
Amesema watajenga uelewa zaidi kwa hadhira kuhusiana na haki za Watoto na Wanawake, ambayo kwao itasaidia kujua namna ya kutatua changamoto zinazowakabili katika jamii inayowazunguka.
No comments: