Benki ya CRDB yazindua kampeni ya “Tupo Mtaani Kwako”

Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts akiwa kwenye gari la CRDB Wakala kuashiria uzindua rasmi wa kampeni ya “Tupo Mtaani Kwako” ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za benki pamoja na kuwaunganisha Watanzania walio wengi kutumia huduma za Benki yao ya CRDB. Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Mashariki Benki ya CRDB, Badru Idd.
Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts akizungumza na waandhishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Tupo Mtaani Kwako” ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za benki pamoja na kuwaunganisha Watanzania walio wengi kutumia huduma za Benki yao ya CRDB. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Kadi wa Benki ya CRDB, Farid Seif.
=== === ===

Benki ya CRDB leo imezindua kampeni ya “Tupo Mtaani Kwako” ambayo inalenga katika kuhamasisha matumizi ya huduma za benki pamoja na kuwaunganisha Watanzania walio wengi kutumia huduma za Benki yao ya CRDB.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB na kuhudhuriwa na wateja na CRDB Wakala, Afisa Biashara Mkuu wa benki hiyo, Dkt. Joseph Witts alisema kampeni hiyo ya “Tupo Mtaani Kwako” itasaidia kuelimisha wateja juu ya fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB, kutoa elimu na ushauri wa masuala ya fedha, pamoja na kuwaunganisha wateja na huduma zinazotolewa na benki hiyo ikiwamo kufungua akaunti.

“Tukiwa Benki ya kizalendo tunajukumu la kuhakikisha tunasaidia kuboresha maisha ya Watanzania kupitia bidhaa na huduma zetu. Kupitia kampeni hii tunakwenda kutimiza wajibu huu kwa kutembelea mtaa kwa mtaa Tanzania nzima kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zinazotolewa na Benki yao,” anasema Dkt. Witts.

Dkt. Witts amesema Benki ya CRDB imejipanga kutumia timu ya wafanyakazi wake wabobevu katika masuala ya kibenki kuwatembelea wateja pale walipo, iwe ni ofisini, sokoni, dukani, stendi na kuwapatia huduma.

“Tutakuwa tukitumia magari yetu haya ambayo mnayaona hapa kuwafikia wateja mtaani, lakini pia tutakuwa na MaGazebo ambayo yatakuwepo mtaani kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wateja,” aliongezea Dkt. Wiits huku akiwataka wateja kutumia fursa hiyo ya kusogezwa kawa huduma karibu kufungua akaunti na kuweka akiba.

Dkt. Witts amesema kampeni hiyo ya ‘Tupo Mtaani Kwako’ pia inalenga katika kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za utoaji huduma ikiwamo CRDB Wakala, SimBanking, Internet Banking na TemboCard. Kupitia njia hizi mteja anaweza kufanya miamala yake ya benki popote pale alipo kwa urahisi, usalama na unafuu.

“… hadi kufikia sasa tuna CRDB Wakala zaidi 17,000nchi nzima ambao wanatoa huduma mtaani, kwahiyo tunaposema Tupo Mtaani Wako, pia tunamaanisha huduma za kibenki karibu zaidi na mteja kupitia CRDB Wakala,” alisisitiza Dkt. Witts huku akibainisha kuwa katika kampeni hiyo wateja watakuwa wakiunganishwa na huduma za SimBanking, Intenert banking na TemboCrad Visa, MasterCard na UnionPay.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki Benki ya CRDB, Badru Idd amewataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo na kuahidi kuwa Benki hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha inamfikia kila Mtanzania. 

“…. tunaanzia katika kanda hii ya Mashariki ambayo inajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar na baadae kusambaa nchi nzima, niwaombe Watanzania wanapoona wafanyakazi wetu mtaani wasisite kuuliza maswali na kuja kupata huduma, hii ni Benki yao na sisi tupo tayari kuwahudumia,” amesema Badru.

Badru amesema katika kipindi hiki Benki ya CRDB pia itaendelea kelimisha wateja na Watanzania kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuweka akiba kupitia kampeni ya “Jipe Tano” ambayo imezinduliwa mwezi Oktoba. 

Kampeni hiyo ya ‘Jipe Tano’ inatoa fursa kwa wateja kujishindia zawadi ya shilingi elfu tano kila wanapoweka akiba katika akaunti zao ikiwamo akaunti ya Watoto Junior Jumbo, Akaunti ya Malkia kwa ajili ya wanawake, Akaunti ya Scholar, Akaunti ya Vikundi ya Niamoja, pamoja na huduma nyengine za uwekaji akiba.

“…. Tumetenga shilingi milioni 100 ambazo zinatolewa kwa washindi 240 kila siku, hivyo niendelee kuwahamasisha wateja waendelee kuweka akiba katika akaunti zao ili wapate nafasi ya kujishindia zaidi na wakati huo huo kutimiza malengo yao,” anasisitiza Badru.

No comments: