BAKWATA YAMPOGEZA RAIS MAGUFULI IKIWATAKA WANASIASA KUKUBALI MATOKEO ILI KULINDA AMANI Inbox
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limempongeza Rais John Mgufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania kwa muhula wa pili na kuwataka Watanzania waendelee kutunza amani wasihamanike sababu ya matokeo ya uchaguzi mkuu.
Pia limewataka wagombea na viongozi baadhi wa vyama vya siasa pamoja na Watanzania kukubaliana na matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), warudi kufanya kazi ya kujenga uchumi na kutafuta riziki halali.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke wakati akizungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu ambapo CCM iliibuka mshindi kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Alisema matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyompa Rais Magufuli kuendelea kukaa madarakani kwa muhula wa pili ni halali na kumpongeza kwa ushindi huo huku akimuombea kwa Mwenyezi Mungu amuongoze na kumjalia hekima ya kuteua wasaidizi watakaokwenda na kasi yake ya kuwatumikia Watanzania kwa utumishi uliotukuka.
“Kwa niaba ya waislamu wa Mwanza, nikiwa Sheikh wa mkoa natoa pongezi za dhati kwa Rais Magufuli na serikali yake kuchaguliwa tena kuiongoza Tanzania,anaheshimu mamlaka na kumtanguliza Mungu kwenye mambo yote lakini rais, wabunge na madiwani waliopatikana ni majibu ya dua zetu sisi waislamu tulimuomba Mwenyezi Mungu atupe kiongozi wa kutufaa,”alisema Sheikh Kabeke.
Alisema yapo yaliyosemwa kuhusu uchaguzi na ifahamike Tanzania ni nchi huru yenye kujiamulia mambo yake, ina kanuni, taratibu na sheria zake, haitafuti uhuru ambao ilishaupata tangu mwaka 1961, hivyo Watanzania na wanasiasa kuendelea kupinga matokeo ni kutoheshimu sheria za nchi na wasihamanike sababu ya matokeo hayo.
Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza alisema wananchi na Watanzania wasihamanike na kuchukua mifumo ya nje baada ya uchaguzi waendelee kutumia mifumo yetu ya kisheria kuimarisha amani kwani uhuru ulishapatikana tangu 1961 kwani kila haki inahitaji msingi wake.
“Dunia leo iko kiganjani tunaona yaliyopita na yanayotokea kwenye nchi zilizokuwa na amani,zilipoingia kwenye vurugu taratibu zote zilivurugika na amani iliharibika pia.Wengi wape, wachache wasikilize na wengi wameamua,tuendelee kuwasikiliza zaidi tukienzi na kulinda amani ya nchi yetu,”alisema Sheikh Kabeke.
Alisema sisi Tanzania tumevuka kwenye uchaguzi kwa amani na tungependa kuona amani hiyo inaendelea kuwepo, kama tunadai haki ama tunataka haki, haiwezi ikawa kama haikuwekewa misingi ya amani ingawa ni kweli amani na haki vinakwenda pamoja,amani ikitangulia na ile haki ikiwepo huifanya amani kutulia.
“Iko hadithi ya Mtume Muhammad S.A.W, ipo dhambi haisameheki kwa hija, sala, sadaka na kufunga,bali mtu aliyelala kwa uchovu akitafuta riziki halali, niwasihi Watanzania wa rika zote, vijana na watu wazima, tukubali matokeo na kurudi kufanya kazi halali baada ya kutangazwa mshindi,naipongeza tume (NEC) uchaguzi ulikwenda vizuri,ndivyo Mwenyezi Mungu alivyokadiria,”alisema Sheikh Kabeke.
Alisistiza ni jambo la kumshukuru Mungu tumeishi kwa amani na utulivu kipindi cha kampeni, kupiga kura na kutangazwa mshindi hadi rais kuapishwa ambapo mkoani Mwanza hali ilikuwa shwari hakuna bomu lililopigwa na kulipongeza jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Pia aliwapongeza waislamu na wasio waislamu, wenye dini na wasio na dini kwa kuwa karibu na viongozi dini kipindi cha uchaguzi ambao waliwaasa kutunza amani wakawaheshimu viongozi hao na kutii hivyo Mwenyezi Mungu awalipe kila la kheri.
No comments: