WATU 12 WAFARIKI DUNIA KUTOKANA MVUA JIJINI DAR ES SALAAM
"
*MAAFA DAR...MVUA YAUA WATU 12,
*AJALI YA MOTO YAUA WATANO WA FAMILIA MOJA
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAAFA makubwa katika Jiji la Dar es Salaam! Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya kuripotiwa watu 12 katika Jiji hilo kufariki dunia kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha huku wengine watano wa familia moja wakiwemo wanafunzi wanne wakifariki kwa ajali ya moto.
Akizungumza leo Oktoba 15,2020,Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambo sasa amewaambia waandishi wa habari kuwa jeshi hilo limepokea taarifa ya vifo vya watu 12 kufariki kutokana na athari ya mvua inayoendelea kunyesha ambapo Oktoba 13, 2020 kuanzia saa 10 alfajiri katika maeneo mbali mbal, mvua kubwa ilianza kunyesha na kuendelea kunyesha mchana kutwa na kusababisha vifo vya watu 12.
Kamanda Mambosasa amesema vifo hivyo vilivyosababishwa na athari za mvua vilitokea katika Mikoa ya Kipolisi Ilala na Kinondoni jijini. Amesema Mkoa wa Polisi Ilala jumla watu 8 walifariki dunia baada ya kusombwa na maji.
"Oktoba 13, 2020 saa moja jioni mwanamke mmoja aliyefahamika kwa majina ya Mariam Yahaya (45), Mkazi wa Vingunguti, alifariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati akijaribu kuokoa vyombo vyake vilivyokuwa vinasombwa na maji.Mwili wake ulikutwa unaelea kando ya mto Msimbazi na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
"Aidha, miili ya watu watano ilipatikana katika bonde la mto Msimbazi eneo la Jangwani, kati ya hao watu wawili walifahamika kwa majina kama
Herieth Kanuti(18), Mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Lutihinda, Ipyana Mwakifuna(19) Mkazi wa Jangwani, Askari Jeshi la akiba la Mgambo na miili mingine ya watu watatu bado haijatambuliwa ikiwa ni wanaume wawili na mwanamke mmoja,"amesema.
Pia amesema tukio lingine la kifo limeripotiwa Oktoba, 14,2020 , saa 12 asubuhi huko Tabata,ambapo mwili wa mtu mmoja mwanaume aliyefahamika kwa majina ya Philipo Feliciani(30), Mkazi wa Tabata Kimanga, ulionekana ukiwa umenasa kwenye matope katika mto Tenge, ambaye alifariki dunia Oktoba 13,2020 , saa 12 jioni baada ya kudondoka na kusombwa na maji.
Amesema mtu huyo alikuwa akijaribu kuvuka kwenye kidaraja cha waenda kwa miguu kilichopo Tabata Kimanga na mwili wa mtu mmoja mwingine mwanaume asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 hadi 35 alikutwa akiwa amefariki dunia katika eneo la Ukonga sabasaba mji mpya.
Kamanda Mambosasa amesema kwa Kinondoni jumla ya watoto wawili wa familia moja na watu wazima wawili walifariki dunia kutokana na athari za mvua.Amewataja waliofariki ni Ibrahim Hassani(24),Mkazi wa Kigogo Buyuni,Hussein Awadhi (5) Mkazi wa Kigogo Buyuni na
3. Bakari Awadhi (14), Mkazi wa Kigogo Buyuni.
Ameongeza watoto hao walifariki dunia kwa kusombwa na maji baada ya nyumba yao iliyopo katika bonde la Kigogo kujaa maji na watoto hao kushindwa kujiokoa na marehemu Ibrahim Hassani alijaribu kumuokoa mtoto mmoja lakini na yeye akasombwa na maji na kufariki dunia.
Pia mnamo 14 Oktoba, 2020, saa mbili asubuhi huko Mabibo mwili wa mtu mmoja mwanaume asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30-35 ulionekana unaelea kwenye mfereji unaopeleka maji katika mto Msimbazi.
Miili ya marehemu imehifadhiwa hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio lingine Kamanda Mambosasa amesema watu watano wa familia moja wamefariki dunia kwa ajali ya moto jijini Dar es Salaam.
"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linasikitika kuthibitisha kutokea kwa ajali ya Moto na kusababisha vifo vya watu watano wa familia moja.Oktoba 13/10/2020 saa nne kamili usiku huko maeneo ya Pugu nyumba yenye vyumba vinne inayomilikiwa na Edward Katema (37),Mfanyabiashara , Mkazi wa Pugu ,iliteketea kwa moto na kusababisha vifo vya watu wa familia moja,*amesema.
Amewataja waliofariki kwa ajali hiyo ni Jackline Frank (27),Mwanafunzi wa Pugu Sekondari.
2. Esther Jeremiah Katemi(15),Mwanafunzi wa Pugu Sekondari, Edward Katemi(11),Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Pugu,Edson Edward Katemi(10) ,Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Green Hill pamoja na Ivon Edward Katemi, mtoto wa miaka 4.
"Chanzo cha moto ni hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye main switch na miili ya marehemu imeifadhiwa hospitali ya Taifa Muhimbili,"amesema Kamanda Mambosasa.
No comments: