Wananchi wametakiwa kuwa ari ya kuanzisha na kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao

Mwezeshaji Charles Makoi akiwapa utaratibu washiriki katika semina namna ya kuchangia mawazo

Na Woinde Shizza, Michuzi TV ARUSHA

TUKIJIWEKEA mikakati ya kujenga zahanati lazima vitendo vyetu vitafsiri malengo ya kuwa na zahanati, hata wadau wa maendeleo wanapokuja kutusaidia basi wakute tumeshaanza ujenzi.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Karatu Abbas Kayanda katika kikao cha ndani na wazee wa kimila (Malagwanani) katika Kijiji Cha  Lositete ,ambapo alisema serikali imetoa kiasi cha Million 150  wilaya ya Karatu kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma  katika  zahanati ya Jobaj, Mang’ola juu, na zahanati ya Huduma. 


Alisema zahanati zote hizo zimejengwa na vijiji husika mpaka sasa kuna zahanati tano wilayani Karatu  ambazo ni Bashay, G-arusha, Sumawe Mahhahha na Marera tayari zimeshakamilika na zinasubiria kufunguliwa baada ya kumaliza usajili na kufafanua kuwa  Wilaya ya Karatu inapata bajeti ya  million 450  kutoka serikalini kwa ajili ya madawa kila mwaka.

Akizungumzia kuhusu usambazaji  wa umeme vijijini Kayanda alisema serikali imevunja mkataba na mkandarasi wa awali wa usambazaji wa umeme (REA three) round one ambaye alitakiwa kumaliza kazi tarehe 30 mwezi wa nane baada ya kushindwa kuendana na makubaliano ya mkataba.  

Alisema hivi sasa Tanesco inafanya tathimini ya mradi mzima ili waweze kumalizia, maeneo yaliyobakia, huku akiwahakikishia wazee wa kimila wa Lositete kwamba umeme utafika Lositete kwa sababu kijiji cha Lositete kipo ndani ya Mpango wa kusambaza umeme.  

Alisema vijiji ambavyo havikuingia kwenye awamu hii vitawekwa kwenye umeme wa (Rea three round two) na utasambazwa kwenye taasisi zote za serikali kama shule zahanati na ofisi za kijiji.

Kuhusu barabara  Kayanda alisema barabara ya Lositete lazima itakarabatiwa kwa sababu tayari iko kwenye bajeti ya mwaka huu ,Utengenezaji  wa barabara za vijini unasimamiwa na wakala wa barabara vijijini (Tarura)ambapo aliwashukuru wazee wa kimila kwa kudumisha hali ya  ulinzi na usalama,nakuongeza kuwa  wazee wamekuwa imara kuwaelekeza vijana mambo ambayo serikali inawahitaji kufanya.

Pamoja na kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Karatu  alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Lositete ambao walikuwa katika mkutano wao mkuu wa kijiji, pamoja na mambo mengine aliwahidi kuendelea kushirikiana nao alisema uongozi si kuongoza peke yako lazima kushirikiana na wananchi katika kuongoza.

Awali katika salamu zao wazee wa kimila walimueleza  Mkuu wa wilaya furaha yao kwa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu Waziri Mourice aliyewaahidi wanakijiji wa Lositete kiasi cha million 7.7 kwa ujenzi wa matundu ya vyoo shule ya msingi Lositete, ukarabati wa majengo  matatu ya nyumba za walimu na kukubali kuwalipia  mshahara walimu wa ziada wapatao wanne wa muda wa miezi miwili mwezi November na Desemba.

No comments: