WABUNGE ACT-WAZALENDO WAWAJIA JUU VIONGOZI WA CHAMA CHAO,WAPINGA VIKALI KAULI YA KUUNGA MKONO MGOMBEA URAIS WA CHADEMA TUNDU LISSU.

WAGOMBEA wawili wa kiti cha Ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo kupitia majimbo ya Kibamba jijini Dar es Salaam na Kyerwa mkoani Kagera wamewajia juu viongozi wa chama hicho kutokana na kauli yao ya kumuunga mkono mgombea wa kiti cha Urais kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu.

Wakizungumza katika mkutano wao na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Wagombea hao Mwesigwa Siraji wa Kibamba na Ntareyeiguru Frederick wa jimbo la Kyerwa, kwa pamoja walisema kauli ya viongozi wao hao hazikubaliki na kwamba zimekiuka misingi ya katiba ya chama hicho.

Alisema wakiwa kama wagombea na wanachama wa chama hicho, hawawezi kulazimishwa ghafla 'kumpigia' debe Lissu hali yakuwa chama hicho kinaye mgombea wake wa nafasi hiyo ya Urais Bernard Membe ambaye kwa mujibu wao anakubalika maeneo mengi nchini.

"Kwa utafiti tulioufanya Membe atapata ushindi mkubwa kutokana na kukubalika na wananchi wengi, cha kushangaza wao wanamuacha na kushinikiza watu tumuunge mkono Lissu" alisema Siraji

Alisema kwa mujibu wa kifungu kilichopo ukurasa wa 21 wa katiba ya ACT Wazalendo, ni kinyume na utaratibu kwa mwanachama yoyote kumuunga mkono au kumpigia debe mtu kutoka chama kingine ambapo kwa kufanya hivyo mtu huyo anakuwa amejifuta uanachama ndani ya chama hicho.

Alisema kwa misingi hiyo, Kiongozi Mkuu wa Chama hicho Zitto Kabwe pamoja na Mwenyekiti wao Maalim Seif Sharif Hamad wanakosa sifa za kuwa wanachama wa ACT-Wazalendo kwa kitendo chao cha kumnadi mgombea wa Urais wa CHADEMA Tundu Lissu.

"Kutokana na hatua hiyo tumepanga jumatatu tutakwenda kufungua kesi mahakamani kule Zanzibar ili ichukue hatua ya kumvua Maalim Seif nafasi yake ya kugombea Urais kutokana na kukosa sifa" aliongeza Siraji

Kwa upande wake Frederick alisema wao kama wanachama wa chama hicho wanalaani kitendo cha viongozi hao kuamua kumkacha mgombea wao Membe hali ya kuwa walimpitisha wao kuwania urais kupiti chama hicho.

"Isitoshe Membe alishiriki kwa ziadi ya asilimia 75 kuandaa ilani ya chama ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu, leo wanajitokeza hadharani kusema hawamtambui, hiyo siyo kweli sisi bado tupo naye hadi mwisho wa uchaguzi" alisema Frederick

Alisema wao kama wabunge wanaendelea kumuombea kura Membe katika majukwaa yote wanayosimama na imani yao ni kwamba atashinda kiti hicho licha ya hujuma anazofanyiwa na viongozi hao wa juu wa chama hicho.

Aidha kwa pamoja walikionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kisitarajie mteremko katika nafasi zote kwa kuwa chama hicho kimejipanga kikamilifu kuhakikisha kinaibuka na ushindi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Pichani kulia ni Mgombea Ubunge wa jimbo la Kibamba kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo,Mwesigwa Siraji akionesha kitabu cha Katiba yao ya chama hicho mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani), ambayo amedai kuwa viongozi wake wa juu wanaikiuka na wao hawatokubali.Mwesigwa amesema kuwa wakiwa kama wagombea na Wanachama wa chama hicho,hawawezi kulazimishwa ghafla kumpigia debe Mgombea Urais wa CHADEMA,Tundu Lissu hali ya kuwa chama chao kina Mgombea Urais Ndugu Bernad Membe anaetambulika kisheria.Kushoto ni Mgombea Ubunge wa jimbo la Kyerwa,Ntareyeiguru Frederic.
Mgombea Ubunge wa jimbo la Kyerwa,Ntareyeiguru Frederic akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani),kuhusu kulaani kitendo cha viongozi wa chama hicho kuamua kumkacha mgombea wao Mhe,Membe hali ya kuwa walimpitisha wao kuwania urais kupiti chama hicho."Isitoshe Membe alishiriki kwa ziadi ya asilimia 75 kuandaa ilani ya chama ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu, leo wanajitokeza hadharani kusema hawamtambui, hiyo siyo kweli sisi bado tupo naye hadi mwisho wa uchaguzi" alisema Frederick

No comments: