Usajili Kili Marathon 2021 wafunguliwa rasmi

 

Washiriki wanaweza kujisajili kwa njia ya mtandao au Tigopesa

Waandaaji wa mbio maarufu ndani na nje ya nchi Kilimanjaro Premium Lager Marthon wametangaza kuanza kwa usajili wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Februari mwakani.

Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji hao, usajili ulianza rasmi Ijumaa Oktoba 16, 2020 ambapo washiriki watatakiwa kujisajili kwa kupitia tovuti yawww.kilimanjaromarathon.com au raia wa Kitanzania au wageni wanaoishi Tanzania wanaweza kujisajili kwa njia ya Tigopesa.

Mkurugenzi wa mbio hizo kitaifa Bw. John Bayo alisema kama miaka yote, kuna idadi maalumu ya washiriki inayohitajika ambayo ikishafikiwa usajili utafungwa kwa mbio zote tatu za  (Kilimanjaro Premium Lager Marathon [42km], Tigo Kili Half Marathon [21km] na Grand Malt 5km Fun Run.

Alisema wanazingatia idadi maalumu ili kuendana na taratibu za Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) ili kuhakikisha usalama wa washiriki na upatikanaji wa huduma muhimu na pia kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ili kujikinga na virusi vya Covid-19.

 “Tunatoa wito kwa washiriki wote wajisajili kwa wakati na kuhakikisha wanalipia ili wathibitishe ushiriki wao,” alisema Bw. Bayo.

Meneja wa Bia ya Kilimanajro Premium Lager na Grand Malt, Irene Mutiganzi alisema wanayo furaha kudhamini kwa mara nyingine mbio hizi ikiwa ni mwaka wa kwanza tangu mlipuko wa virusi  vya Covid-19 ambapo watu wataweza kujumuika tena na kufurahi kwa kupitia michezo,” Tunatoa wito kwa washiriki wajitokeze kwa wingi na kujisajili kwa mbio za 42 km na 5km kwa wakati ili wasikose nafasi,” alisema.

Kilimanjaro Premium Lager imekuwa mdhamini mkuu wa mbio hizi tangu kuanzishwa kwake miaka 19 iliyopita.

Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael, alitoa wito kwa washirki watumie Tigopesa kujisajili kwani imefanya zoezi hili kuwa rahisi ikilinganishwa na hapo awali na kuongeza kuwa wale ambao hawana laini za Tigo wanaweza kuwaomba wenzao wenye laini hizo kuwafanyia usajili.

"Huu utakuwa mwaka wa sita kwa Tigo kudhamini na kushiriki katika mbio hizi maarufu na za kimataifa. Natoa wito kwa washiriki wa Tigo Kili Half Marathon wajisajili kwa kubonyeza *149*20# na kufuata maelezo na kisha kukamilisha usajili wao kwa kulipia kupitia Tigopesa kwa kuwa ni rahisi na salama,” alisema Shisael.

Wadhamini wa mbio za mwakani ni, Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu -42Km) , TIGO (21Km-Half Marathon), Grand Malt (5km –Fun Run), Kilimanjaro Water, TPC Limited, Simba Cement, Absa Bank Tanzania, Unilever – na watoa huduma rasmi ni Keys Hotel, Garda World Security na CMC Automobiles.

Mbio za mwakani zitafanyika Jumapili Februari 28, 2021 katika Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi ambapo mbio zote tatu zitaanzia na kumalizikia.

Mbio hizo zinaratibiwa kitaifa na Kampuni ya Executive Solutions.

No comments: