UJIO WA KOCHA CEDRIC KAZE YANGA SC NA VURUGU ZA DUBE, NI TISHIO KWA MABINGWA SIMBA SC MSIMU HUU?
NAWEZA kusema Msimu wa 2020-2021 wa Mashindano ni msimu mgumu kwa miamba ya Soka nchini Tanzania, hapa nawazungumzia Simba SC, Yanga SC na Azam FC bila kuwasahau wengine wakina Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Tanzania Prisons, Namungo FC, na wengine wengi wanaoshiriki kundumbwe ndumbwe cha Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL).
Timu nyingi zimejipanga kwa kufanya usajili wa aina yake ili kukabiliana kisawa sawa msimu huu wa Mashindano na kuhakikisha zinafanya vizuri katika mashindano husika, iwe kwenye VPL, Kombe la Shirikisho (ASFC) na hata Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho la CAF kwa wanaoshiriki msimu huu wa Mashindano.
Hapa tuangalie zaidi Ubingwa wa Simba SC wa VPL na ASFC kwa msimu uliopita wa 2019-2020, wengi wanaamini Simba SC ilifanya vizuri katika Michuano hiyo kutokana na Kikosi bora kilichoandaliwa, Ndiyo! walifanya vizuri kutokana na Kikosi Bora walichokuwa na nacho msimu huo.
Msimu huu, Je? mambo yatakuwa kama msimu uliopita kwa Simba SC kutwaa mataji yote. Yanga SC walishindwa kufanya vizuri msimu uliopita na hii inaaminika kutokana na kutokuwa na Kikosi bora cha Mashindano kwa Wana Jangwani maana hata Wawakilishi wa Michuano ya Kombe la Shirikisho la CAF ni Namungo FC kutoka Ruangwa mkoani Lindi, baada ya wao kuwa nafasi ya Pili ya Michuano ya ASFC katika Fainali iliyopigwa mjini Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo walipokea kichapo cha bao 2-1 kutoka kwa Simba SC.
Yanga SC msimu huu wameonekana kupania vilivyo katika VPL, ASFC wanaonekana kuwa na hasira sana! Usajili uliofanywa na GSM chini ya Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mhandisi Hersi Said ni balaaa...tunaiona Yanga itakayoleta upinzani mkubwa kwa watani wao Simba SC na hata Azam FC.
Usajili uliofanywa na Yanga wa Kocha Mkuu, Mburundi Cedric Kaze mwenye Leseni ya CAF na mwenye sifa kubwa katika tasni aya Soka ni hatari! ni usajili unaonekana kuwa na mipango zaidi klabuni hapo, hii ni baada ya kuachwa kikosini hapo, Kocha Zlatko Krmpotic bila kumsahau Kocha Luc Eymael alifungwashiwa virago kabla ya kutimliwa Krmpotic.
Tazama usajili wakina Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Carlos Carlinhos, Yacouba Sogne, Michael Sarpong, Farid Mussa Malik, Waziri Junior, Kibwana Shomari, Zawadi Mauya, Bakari Nondo Mwamnyeto, Yassin Mustafa hao wamekutana na kina Lamine Moro, Said Makapu, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Abdulaziz Makame, Ditram Nchimbi ni balaaaa!.
Hii ni ishara kuwa Yanga SC wamepania msimu huu wa Mashindano na huenda ikaleta ushindani mkubwa kwa Simba SC na Azam FC ambao ndio timu zinazopewa kipaumbele kuwania Ubingwa zaidi msimu huu.
Azam FC wamesajili Wachezaji wapya wakiwa chini ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba sio mchezo wana mtu anaitwa Prince Dube mpachika mabao mkubwa kwa sasa kikosini hapo hadi sasa katika michezo Sita tayari amefunga mabao Sita uwiano wa kufunga bao kila mechi! Dube ni Mshambuliaji Bora Azam FC na VPL mpaka sasa katika michezo hii ya mwanzo na kuifanya Azam kuongoza Ligi kwa jumla ya alama 18 katika msimamo. Sijui hatujajua kwenye ASFC msimu huu itakuaje tusubiri tu.
Turudi kwenye Swali letu, Ujio wa Kocha Cedric Kaze na Upachikaji mabao wa Mshambuliaji Prince Dube wa Azam FC hii itakuwa tishio kwa Mabingwa wa VPL, ASFC msimu uliopita, Simba SC ??? Ni swali ambalo lina hitaji majibu ya ninyi wasomaji wa Makala hii ya Michezo.
No comments: