TTB, CLOUDS MEDIA GROUP NA SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION KUSHIRIKIANA KUTAGAZA UTALII WA NDANI
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB Jaji Thomas Mihayo(kushoto)na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Ndege la Precision Air wakiwashuhudia Mindi kasiga (kulia), Mkurugenzi wa Masoko wa TTB na Lilian Massawe wakisaini mkataba wa maelewano katika hafla iliyofanyika katika ofisi za TTB jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB Jaji Thomas Mihayo(kushoto) na Mkurugenzi mkuu wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga wakiwashuhudia Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Mindi kasiga (kulia) na Sheba Kussaga, Mkurugenzi wa Biashara na Mendeleo clouds Media Group wakiweka saini mkataba wa malewano wa miaka mitatu.
Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imesaini mkataba wamakubaliano na kampuni ya Clouds media group pamoja na Shirika la ndege la Precision Air kwa lengo la kuungana pamoja katika kuwahamasisha Watanzania kufanya utalii wa ndani kupitia kampeni ya “Twende Serengeti” inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 16 Oktoba 2020.
Kampeni ya Twende Serengeti imeandaliwa hususani kwa ajili ya watanzania kwenda kuembelea hifadhi ya Serengeti ili kujionea msafara wa nyumbu wanaohama kutoka Tanzania na kwenda nchini Kenya na kurudi tena Tanzania.
Akiongea wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Bi. Mindi Kasiga alisema,
Kampeni ya Twende Serengeti ni moja ya mkakati wa TTB katika kuwafanya Watanzania kujenga utamaduni wa kuvitembelea vivutio vya utalii vya Tanzania.
Aidha, Bi. Kasiga ameongezea kuwa TTB ipo bega kwa bega na wadau wa sekta mbalimbali zikiwamo sekta ya habari na sekta ya usafiri na hilo linadhihirishwa na tukio la uwekaji saini wa mkataba huu wa makubaliano wa miaka mitatu na Clouds Media Group ambao tutatumia chombo hiki katika kuitangaza kamapeni hii.
Bi. Mindi ameeleza kuwa kwa upande wa usafiri, wamesaini mkataba wa makubaliano na shirika la ndege la Precision Air ambalo limetoa ndege mbili kwa punguzo maalum zenye uwezo wa kubeba abiria 48 kutoka Dar es Salaam mpaka Serengeti na kurudi Dar es salaam ambapo watalii wataondoka Dar es Salaam Oktoba 16 na kurudi Oktoba 18.
Mkurugenzi wa Clouds Media group, Bw. Joseph Kusaga ametumia nafasi hiyo kuishukuru TTB kwa kushirikisha wadau wa vyombo vya habari katika kampeni hii ambayo itasaidia kuongeza idadi ya watalii wa ndani.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ndege la Precision Air, Patrick Mwanri amesema kwa kushiriki katika kampeni hiyo itazidi kujenga imani kwa wateja wa ndani na nje ya Tanzania wa shirika hilo la ndege na kuvutia wengi kutumia huduma ya shirika hilo.
Bodi ya Utalii Tanzania imeendelea kufanya kampeni za kuwapeleka watalii wa ndani katika maeneo mengine ya vivutio vya utalii na kuwakaribisha wadau wengine kuunga mkono kwa kushirikiana na TTB katika kampeni zinasofuata. Utalii wa Tanzania unaanza na Mtanzania mwenyewe.
No comments: