TAHADHALI YATOLEWA JUU YA MAGONJWA YA MLIPUKO

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUCHUKUA TAHADHARI NA NJIA ZA KUEPUKA MAGONJWA YA MLIPUKO KATIKA KIPINDI CHA MVUA ZA MASIKA

Ndugu wananchi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutoa tahadhari na njia za kuepuka magonjwa mlipuko kufuatia kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

Kufuatia mvua hizi, ni wazi kuwa uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa kama ya kuhara ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu, na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue, endapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema.

Wote tumeshuhudia kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa miundo mbinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka ambapo hali hii inahatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko.

Ndugu wananchi,
Kwa sababu hiyo, Wizara inapenda kutoa Taarifa na Tahadhari kwa Umma ili kuweza kuchukua tahadhari na kuelekeza njia za kijikinga dhidi ya Magonjwa haya.

Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti magonjwa haya ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu ambao ulikoma mwezi Julai mwaka 2019. Hii inatokana na jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama na ushirikiano mzuri wa wananchi. Hivyo ili tuweze kuandika historia ya kutokomeza kabisa Kipindupindu na magonjwa mengine hatuna budi kukumbushana na kuchukua tahadhari kwa kila Mwananchi, Taasisi na Viongozi Ngazi zote ili kujikinga na kuzingatia kanuni za afya kwa kufanya yafuatayo:-

i. Kuchemsha Maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalumu kama Waterguard n.k kabla ya kuyatumia na kuhakikisha maji ya kunywa na yale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi
ii. Kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama
iii. Kutumia ipasavyo vyoo na kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara hasa:-

- kabla ya kula
- baada ya kutoka chooni
- baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
- baada ya kumhudumia mgonjwa
iv. Kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula
v. Kuongeza usimamizi wa usafi wa jumla na mikono katika maeno ya mikusanyiko kama mashuleni, vyuo, masoko,
vi. Kutotapisha vyoo au kutotiririshaji maji taka
vii. Kujikinga dhidi ya kuumwa na mbu muda wote na kutumia ipasavyo vyandarua viii. Kutoa taarifa na kwenda katika kituo cha kutolea huduma za afya endapo utapatwa na ugonjwa wa kuharisha au kutapika
ix. Kusimamia hali ya usafi katika mifumo ya maji safi, maji taka na mitaro
x. Kutoa taarifa kwenye ofisi za Serikali za mitaa, Maafisa Afya au kupiga simu namba 199 endapo mtu au kikundi cha watu kitafanya shughuli zenye kuashiria uchafuzi wowote wa mazingira.

Aidha, Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wanaelekezwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikaili za mitaa, Wananchi na wadau mbali mbali ili kuhakisha kila eneo lilio chini yao, haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko.

Wizara inaendelea kuwakumbusha kuwa Kinga ni Bora kuliko Tiba tuendeleze mafanikio tuliyopata katika kudhibiti Magonjwa hasa tunapomkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alisimamia kupingana na maadui watatu ikiwemo Maradhi.

Hivyo tuendelee kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka yetu ya hali ya hewa nchini na shime tuimarishe afya zetu kwa kudumisha usafi wa mazingira na tabia za usafi katika familia na jamii yetu kwa ujumla ikiwemo kudhibiti mazalia ya mbu.

Imetolewa na
Prof. Abel Makubi- Mganga Mkuu wa Serikali
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto
Dodoma, 15 Oktoba 2020

No comments: