NYUMBA ZA MAKAZI MAGOMENI KOTA KUKAMILIKA JANUARI 2021
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Arch. Elius Mwakalinga akiwa ameambata na Mtendaji mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daudi Kondoro wakikagua mradi wa makazi ya Magomeni kota uliokamilika kwa asilimia 81 na hadi kufikia Januari mwakani zitakuwa zimekamilika na kuwa tayari kwa makazi, leo jijini Dar es Salaam.
Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Arch. Elius Mwakalinga akizungumza na wajasiriamali wanaonufaika kupitia ujenzi wa mradi huo wa makazi wa Magomeni kota jijini Dar es Salaam.
*Zakamilika kwa asilimia 81.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
IMEELEZWA kuwa mradi wa nyumba za makazi ya wakazi wa Magomeni kota jijini Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 81 na hadi kufikia Januari mwaka ujao nyumba hizo zitakuwa tayari kutumika kwa makazi.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchunguzi na Mawasiliano Arch. Elius Mwakalinga amesema kuwa mradi huo uliozinduliwa na Rais Dkt.John Magufuli mnamo Aprili 15, 2017 umekamilika kwa asilimia 81 na kaya 656 zinatarajiwa kuishi katika kota hizo zilizojengwa kisasa pamoja na kusogezewa huduma muhimu za kijamii.
"Hadi sasa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) wameletewa fedha zote za kukamilisha mradi huu hivyo ni vyema wakatumia muda uliobaki kukamilisha sehemu iliyobaki ili wananchi wahamie sehemu hii ambayo Serikali imejenga kwa kiasi kikubwa cha fedha katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira bora zaidi." Ameeleza.
Amesema kuwa katika eneo hilo la makazi miundombinu imejengwa kwa umakini wa hali ya juu hasa kwa kuzingatia miundombinu ya umeme, maduka, maeneo ya michezo pamoja na huduma za kifedha.
Aidha amesema kuwa mpango huo ni endelevu katika maeneo mbalimbali nchini na hiyo ni katika kuhakikisha wananchi wananchi wanaishi katika mazingira bora na kupata mahitaji ya msingi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daudi Kondoro amesema kuwa, kazi za ujenzi wa nyumba hizo hufanywa usiku na mchana na malighafi zote zinanunuliwa katika viwanda vya ndani.
Amesema, gharama za utekelezaji wa mradi huo hadi kufika mwezi Oktoba mwaka huu umefika zaidi ya bilioni thelathini na tatu na asilimia 19 zilizobakia zitakamilika mwezi ifikapo Januari mwaka ujao.
Vilevile amesema kuwa, Wakala hiyo imekuwa ikifuatilia kwa karibu katika kuhakikisha malengo ya mradi huo yanafikiwa katika ubora, viwango, vipimo, gharama na muda ili kukamilisha kwa wakati miradi ya aina hiyo.
Mradi huo wa ujenzi wa nyumba za makazi uliogharamiwa na Serikali na kusimamiwa na TBA unajumuisha nyumba za makazi yenye huduma zote za kijamii na miundombinu muhimu,na licha ya kuchelewa kwa miaka miwili, Januari mwaka ujao nyumba hizo zitakuwa tayari kwaajili ya makazi.
No comments: