NMB yashinda tuzo ya benki salama zaidi nchini kwa mwaka 2020

 

 

Benki ya NMB imeshinda tuzo ya umahiri baada ya kuibuka benki salama zaidi Tanzania kwa mwaka 2020.

Tuzo hizo zimetolewa Jumatatu tarehe 20 Oktoba, 2020 na Jarida la kimataifa la Global Finance la jijini New York, Marekani lililojikita katika uchapishaji wa habari za masoko ya fedha na mitaji ulimwenguni.

Tuzo za benki salama zaidi hufanyika kila mwaka kwa kila bara na kwa kila nchi duniani na hutolewa baada ya kufanyika tathmini ya kina kwa kuzingatia viwango vya makampuni ya Moody’s, Standard & Poor’s na Fitch - vigezo hivi ni vya kimataifa vinavyotoa taarifa za afya za mabenki na uwezo wa makampuni kujiendesha.

Tuzo hii imekuja miezi michache tu baada ya Benki ya NMB kutunukiwa tuzo ya kuwa benki bora zaidi Tanzania kwa mara ya nane mfululizo na Jarida la Euromoney lenye makao makuu jijini London nchini Uingereza linalochapisha habari za masoko ya fedha na mitaji pia.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema: “Ni heshima kubwa kwetu kutambulika kama benki salama zaidi na yenye uwezo wa kuendelea na biashara kuleta faida kwa wanahisa wetu na nchi kwa ujumla. Tuzo hii ni ishara ya uimara wa Benki ya NMB kuhudumia wateja katika soko lenye ushindani na mazingira yanayobadilika kila wakati.  Wakati wasiwasi wa janga la Covid-19 ukiendelea kuisumbua dunia, tuzo hii inadhihirisha uimara, utulivu na kasi yetu ya kubadilika kiteknolojia kuwawezesha wafanyakazi, wateja wetu na watanzania kwa ujumla kufanikisha malengo yao ya kiuchumi.”

Zaipuna amesema tuzo hii inaonyesha juhudi kubwa ya Benki ya NMB kutoa huduma bora na salama kwa wateja wake kwa viwango vya kimataifa na kuweka mustakabali wa huduma za kibenki nchini.

Taarifa za fedha za Benki ya NMB zinaonyesha kwa mwaka 2019 benki ilipata faida ya TZS 142 bilioni baada ya kodi ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 46 kutoka TZS 98 bilioni iliyopata mwaka uliotangulia hivyo kuifanya iendelee kuwa benki inayopata faida kubwa zaidi nchini kwa zaidi ya muongo mmoja sasa. Kwa sasa mali za benki ya NMB zimefikia Zaidi ya shilingi trilioni 7.  Miongoni mwa wanahisa wa Benki ya NMB ni Rabobank yenye asilimia 34.9 pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye asilimia 31.8.

Joseph D. Giarraputo, Mhariri Mkuu wa Jarida la Global Finance amesema: “Janga la corona limeathiri sehemu kubwa ya biashara kwa mwaka 2020 hivyo kufanya utabiri na makisio duniani kuwa mgumu; lakini biashara lazima iendelee. Benki ya NMB ni mfano wa taasisi iliyokuwa imejipanga kuinuka na kuchangamkia fursa za kutoa  huduma mbadala za kibenki kidijitali katika kipindi cha janga la corona hivyo kuwa salama hata sasa. Matokeo ya tuzo hii yatatumiwa na kampuni kubwa, wawekezaji hata watu binafsi kupima usalama wa benki wanayopenda kufanya nayo biashara.” 

No comments: