NAIBU KAMISHNA MKUU TRA: ZINGATIENI SHERIA ILI MTOZE KODI STAHIKI
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kushoto) wakati Naibu Kamishna Mkuu huyo alipomtembelea ofisini kwake kumshukuru kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na uongozi mzima wa mkoa huo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Kulia ni Meneja TRA Mkoa wa Dodoma Bi. Kabula Mwemezi
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo wakati Naibu Kamishna Mkuu huyo alipomtembelea ofisini kwake kumshukuru kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na uongozi mzima wa mkoa huo kwa Mamlaka hiyo.
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Bi. Sezaria Makota wakati Naibu Kamishna Mkuu huyo alipomtembelea ofisini kwake kumsalimia na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri unaotolewa na uongozi mzima wa wilaya hiyo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Bi. Sezaria Makota akizungumza na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati Naibu Kamishna Mkuu huyo alipomtembelea ofisini kwake kumsalimia na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri unaotolewa na uongozi mzima wa wilaya hiyo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo akizungumza na watumishi wa Ofisi ya TRA Mkoa wa Dodoma wakati Naibu Kamishna Mkuu huyo alipowatembelea kwa lengo la kuwapa hamasa watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo akizungumza na watumishi wa Ofisi ya TRA Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma wakati Naibu Kamishna Mkuu huyo alipowatembelea kwa lengo la kuwapa hamasa watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Bw. Sadru Kamugisha akizungumzia mafanikio ya utendaji kazi wa ofisi yake wakati Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Msafiri Mbibo alipotembelea wilaya hiyo kwa lengo la kuwapa hamasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika ukusanyaji mapato ya Serikali. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).
………………………………………………………………………………
Na Veronica Kazimoto,Dodoma
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo amewahimiza watumishi wa mamlaka hiyo kusoma na kuzingatia sheria za kodi ili kuhakikisha kuwa wanatoza kodi stahiki.
Akizungumza hivi karibuni na watumishi wa ofisi ya TRA Wilaya Kondoa na Dodoma mjini wakati akihitimisha ziara yake mkoani hapa, Naibu Kamishna Mkuu huyo aliwaambia kwamba, ni wajibu wa kila mmoja wao kutenga muda kwa ajili ya kusoma sheria na kuzielewa vizuri ili iwe rahisi kuzitekeleza.
“Kodi haiwezi kukusanywa wala haiwezi kuachwa kukusanywa mpaka pawepo maelekezo ya sheria. Hivyo, usalama wenu katika kukusanya kodi ni lazima msome na kuzingatia sheria zote za kodi zinazosimamiwa na TRA ndipo mtakapoweza kutoza kodi stahiki na kutekeleza majukumu yenu ipasavyo,” alisema Bw. Mbibo.
Naibu Kamishna Mkuu huyo aliongeza kuwa, suala la kujua na kuzingatia sheria za kodi vizuri linaenda sambamba na kuwaelimisha walipakodi kuhusu sheria hizo na siyo kuachia jukumu hilo kwa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi peke yake.
“Watumishi mlio wengi mnajua kazi ya kuelimisha walipakodi ni jukumu la Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi tu, naomba niwaambie kwamba, suala hili ni la kila mtumishi ndani ya TRA na ndio maana ninawasisitiza kusoma, kuelewa na kuzingatia sheria vizuri ili muweze kuwaelimisha wateja wetu na hatimaye waweze kuongeza uhiari katika ulipaji kodi,” alisisitiza Naibu Kamishna Mkuu.
Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma Bi. Kabula Mwemezi alimshukuru Naibu Kamishna Mkuu huyo kwa kufanya ziara katika ofisi zote za TRA mkoani hapa na kuahidi kuendelea kuwasisitiza watumishi kujenga tabia ya kusoma sheria na kuongeza kuwa, atakikisha watumishi hao wanapewa mafunzo ya mara kwa mara kwa dhumuni la kuwajengea uwezo katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
“Napenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa kutembelea ofisi zote za TRA hapa mkoani Dodoma na ninakuahidi kwamba mimi pamoja na viongozi wenzangu wa mkoa tutaendelea kuwakumbusha watumishi kusoma sheria na kuzielewa vizuri na pia tutahakikisha wanapata mafunzo ya kuwajengea uwezo katika ukusanyaji mapato kila mara,” alisema Bi. Mwemezi.
Mbali na kukutana na watumishi wa TRA katika ziara yake, Naibu Kamishna Mkuu Mbibo alifanikiwa pia kumtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Suleiman Serera, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa Bi. Sarah Komba.
Lengo la kuwatembelea viongozi hao ilikuwa ni kuwasalimia na kuwashukuru kwa ushirikiano mkubwa wanautoa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambao umechangia katika kufanikisha ukusanyaji mapato ya Serikali hapa nchini.
Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Msafiri Mbibo amehitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Dodoma iliyoanza tarehe 12 hadi 17 Oktoba, 2020 ambapo kila ofisi ya TRA aliyoitembelea mkoani hapa, alihakikisha anawaasa watumishi wote wa ofisi hizo kufanya kazi kwa bidii, weledi, kuzingatia maadili na kuwa na heshima kwa watu wote.
No comments: