MIAKA 10 NA MAFANIKIO LUKUKI YA KLINIKI YA HEAMEDA



Mkurugenzi Mkuu na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Kliniki ya moyo ya Hemaeda Dkt. Henry Mwandolela akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi na wajumbe wa bodi ya kliniki hiyo wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, leo jijini Dar es Salaam. 
Mkurugenzi Mkuu na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Kliniki ya moyo ya Hemaeda Dkt. Henry Mwandolela akizungumza na Michuzi Tv katika maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kueleza kuwa lengo kuu la kliniki hiyo ni kuwa hospitali ya hadhi na ubora wa hali ya juu ili kuokoa maisha ya watanzania na kutoa huduma nzuri za afya kwa wananchi, leo jijini Dar es Salaam.



Huduma zikiendelea katika kliniki ya moyo ya Heameda, Bunju B jijini Dar es Salaam.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

IKIWA  moja ya Kliniki kubwa inayotoa huduma za Afya kwa jamii hasa kwa magonjwa ya moyo Heameda Specialized Polyclinic, wameadhimisha miaka kumi ya utoaji huduma kwa jamii ya watanzania tangu ilipoanzishwa Oktoba 20, 2010 huku wakisherekea mafanikio makubwa ya kutoa huduma bora na kuwafikia na kuwahudumia  wagonjwa wapatao kumi na sita elfu.

Akizungumza na Michuzi TV wakati wa hafla hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kliniki hiyo na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Dkt.Henry Mwandolela amesema, tangu kuanzishwa na kusajiliwa rasmi  kwa mujibu wa Sheria za nchi chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Kliniki hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, magonjwa ya  wanawake, ngozi, masikio, pua, figo na koo.

"Haemeda imekua ikizingatia utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia ubora wa hali ya juu...tuna wataalamu wabobevu pamoja na vifaa vya kisasa vinavyotumika kuhudumiwa wagonjwa na kwa ufanisi wa hali ya juu." Amesema.

Dkt. Mwandolela amesema kuwa, lengo la kliniki hiyo ni kuwa hospitali yenye hadhi na ubora wa hali ya juu katika kuokoa maisha ya watanzania katika sekta ya afya.

"Tunaishukuru Serikali kwa kuwa pamoja na sisi tangu tulipoanza hadi sasa, matarajio yetu ni kuendelea kuboresha huduma za wagonjwa wa nje (OPD,) Kuboresha vipimo vyote muhimu, kuboresha huduma za dharura, huduma za kulaza wagonjwa, upasuaji na kulaza wagonjwa mahututi." Ameeleza.

Amesema kuwa katika miaka 10 ya utendaji kazi wao mafanikio makubwa wanayojivunia ni kuwafikia na kuwahudumia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali, na kuahidi kuendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutoa elimu kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza na yaambukizayo.

Kuhusiana na hali ya ugonjwa wa moyo katika Kliniki hiyo, Dkt. Mwandolela amesema, asilimia 70 ya wagonjwa walioonwa na kufanyiwa vipimo walithibitika kua magonjwa ya moyo hasa shinikizo la damu.

"Tatizo hili la shinikizo la damu hasa husababishwa na kurithi, kwa wazazi wenye tatizo hili kuna uwezekano wa asilimia 90 kuzaa mtoto mwenye tatizo hilo, na tatizo hili huanza kuonekana kuanzia miaka 40 na kuendelea na wengi huja hospitalini wakiwa katika hatua ya juu zaidi ambazo hupelekea athari kwa viungo vingine kama figo na moyo kutanuka." Ameeleza Dkt. Mwandolela.

Amesema kuwa wataalamu wa Afya kutoka Kliniki hiyo wamekuwa wakitoa elimu ya afya na upimaji kwa wananchi, wafanyakazi wa Taasisi za Umma na binafsi na hiyo ni pamoja na kushiriki katika maonesho ya biashara (Sabasaba,) kwa kutoa elimu bure na kufanya uchunguzi wa kiafya na tayari wamefanya kambi mbalimbali za uchunguzi wa afya bure kwa wananchi kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoa nchini na India.

Aidha amewataka wananchi kutembelea kliniki hiyo iliyopo Bunju B, Manispaa ya Kinondoni karibu na nyumba za TBA, na kupata huduma bora na kwa gharama nafuu.

No comments: