MGOMBEA WA CCM JIMBO LA SGD KASKAZINI AAHIDI KUONDOA CHANGAMOTO YA HUDUMA ZA AFYA KWA WAJAWAZITO


Na Jumbe Ismailly- SINGIDA


MGOMBEA ubunge mteule wa jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Ramadhani Abedi Ighondo ameahidi kwamba endapo atapata ridhaa ya kuwa Mbunge wa jimbo hilo,atahakikisha wanawake wa jimbo hilo wanaondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Mgombea huyo kwa tiketi ya Cham Cha Mapinduzi (CCM) alitoa ahadi hiyo katika mikutano yake tofauti ya kampeni za uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi huu aliyoifanya katika vijiji vya Mwachambia na Mvae,wilayani Singida.

Aidha Ighondo alisisitiza kwamba hakuna kitu ambacho kinatesa sana wananchi kama upatikanaji wa huduma za afya kwani huduma hizo zinapokuwa mbaya anayeumia zaidi ni mama, watoto pamoja na watoto wa kike wanaposafirishwa kwa usafiri wa tela la ng’ombe wanapohitaji huduma za kujifungua.

“Jamani tuondoe hizi adha zinazotukabili dada zangu wameongea maneno ya uchungu sana mimi msema kweli nilikuwa nabubujikwa na machoji,kwani hakuna kitu kinachotesa sana kama huduma za afya anayeumia ni mama,anayeumia ni mtoto pamoja na watoto wa kike wanapohitaji huduma za kujifungua”alifafanua Ighondo.

Alisisitiza mgombea huyo kwamba mwanamke anaposafirishwa kwa kutumia usafiri wa tela la ng’ombe na kisha kwa bahati mbaya anapoteza maisha yake akiwa anjiani kwenda kwenye huduma za afya kwa ajili ya kwenda kujifungua ni aibu kubwa sana hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wamuunge mkono ili aweze kuwatatulia changamoto hiyo.

“Amesema sana kaka yangu Elia kuhusu jitihada tuliziofanya kuhusu hii zahanati yetu,inaweza ikawa ni vigumu mimi kujielezea,lakini maneno aliyozungumza kaka Elia yanatosha na hamna budi kuyaamini kuwa ni ya kweli”aliweka bayana Ighondo.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwachambia,Filbert Ntandu alisema miaka 12 wananchi wa Kijiji cha Mwachambia wamekuwa wakitembea umbali wa kati ya kilomita nane hadi 12 kufuata huduma za upatikanaji wa afya.

Aidha Ntandu alifafanua pia kuwa baada ya serikali kuu kuagiza kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati lakini pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwachambia kukamilisha ujenzi huo kwa nguvu zao,mpaka sasa hakuna huduma zinazotolewa kutokana na jengo hilo kutokuwa na milango na madirisha.

“Kina mama wanahangaika sana licha ya zahanati hiyo kukamilika muda mrefu baada ya agizo la serikali kuu kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati wananchi wa Mwachambia wamejitahidi kuanzia mwaka 2012 mpaka sasa hivi jengo hili limefikia hatua ya kuweka milango,madirisha na sakafu juu wameshapaua”alisisitiza Mtendaji huyo.

Hata hivyo Ntandu aliiomba serikali kuu iwasaidie wananchci hao ili waweze kuanza kupatiwa huduma za afya kwenye majengo hayo yaliyoshindwa kukamilishwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na waziri wa maliasili na utalii,Lazaro Nyalandu katika kipindi chake cha uongozi wa takribani miaka 17.

“Shida ni madirisha,milango pamoja na sakafu juu wameshapaua tunaiomba serikali kuu iwasaidie ili waanze kutibiwa mwezi januari,mwakani”alibainisha Ntandu ambaye pia ni mlinzi wa amani wa Kijiji cha Mwachambia.

Kwa mujibu wa afisa mtendaji huyo wananchi wa Kijiji cha Mwachambia hivi sasa hufuata huduma za afya umbali wa takribani kilomita 12 hadi Kijiji cha Msange na kilomita nane hadi Kijiji cha Mdilu na kwamba wanapochelewa kurudi nyumbani hutukanwa na waume zao.

Tatu Rajabu ni mkazi wa Kijiji cha Mwachambia aliweka bayana kwamba yeye kama mwanamke anaona changamoto kubwa inayowakabili akina mama ni huduma za afya,hususani kwa wanawake wajawazito ambao wamekuwa wakijifungua njiani kutokana na kufuata huduma hiyo umbali mrefu.

Kampeni meneja wa mgombea ubunge jimbo la Singida Kaskazini,Elia Digha(wa kwanza kutoka kushoto) akiwanadi wagombea ubunge na udiwani katika Kijiji cha Mwachambia,Kata aya Maghojoa,Singida Vijijini.
Jengo la zahanati ya Kijiji cha Mwachambia,Kata ya Magahojoa lililotelekezwa na aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii na mbunge wa ajimbo la Singida Kaskazini,Lazaro Nyalandu kwa kipindi cha miaka 12 sasa tangu wananchci walipokamilisha ujenzi na kufikia hatua hiyo.
(Picha zote Na Jumbe Ismailly)

No comments: