MAKALA YA JUBILEI YA MIAKA 25 YA UPADRE PATERNI JIMBO KATOLIKI LA SINGIDA
Padre Dkt. Paterni Mangi (katikati) akiendelea na misa takatifu ya kumshukuru Mungu kwa miaka 25 ya utume wa upadre iliyofanyika Oktoba 17, 2020 katika Parokia ya Mt. Joseph Mfanyakazi Mandewa Jimbo Katoliki la Singida. Wa kwanza kulia ni Padre Jonas Mlewa na Padre Aloyce Kijanga (kushoto).
Padre Dkt. Paterni Mangi (wa tatu kushoto mstari wa mbele) akwa katika picha ya pamoja na mapadre wenzake mara baada ya misa takatifu ya kumshukuru Mungu Mungu kwa miaka 25 ya utume wa upadre iliyofanyika Oktoba 17, 2020 katika Parokia ya Mt. Joseph Mfanyakazi Mandewa Jimbo Katoliki la Singida.
*************************************
Eleuteri Mangi
Jubilei ni tukio la furaha, ni tukio la shangwe kubwa inayoshirikisha watu wengi ambao wanakuja kufuatia wito wa baragumu linalopigwa kama Yobel iliyopigwa na wana wa Israeli.
Kanisa Katoliki kwa kufuata desturi ya Taifa teule limekuwa na desturi ya kufanya Jubilei ya miaka ishirini na tano (Jubilei ya Fedha), Jubilei miaka hamsini (Jubilei ya Dhahabu), Jubilei ya miaka sabini na tano (Jubilei ya Almasi), Jubilei ya miaka mia na Jubilei ya miaka elfu moja.
Padre Dkt. Paterni Mangi Oktoba 15 na 17, 2020 amemshukuru Mungu kwa Jubilei ya miaka ishirini na tano (Jubilei ya Fedha) kwa utume wake kwa kulitumikia kanisa Jimbo Katoliki la Singida. Oktoba 15 aliadhimisha misa takatifu katika Kigango cha Mvae alipozaliwa ambapo misa hiyo ilihudhuriwa na Mhashamu Askofu wa jimbo hilo Askofu Edward Mapunda, Mapadre, watawa na waumini wa parokia ya Ilongero pamoja na wageni waalikwa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika Ibada hiyo Askofu Edward Mapunda aliwashukuru mapadre, watawa na waumini wote waliohudhuria ibada hiyo na kuwahimiza kuendelea kuwa imara katika kuisimamia na kulinda imani ya kanisa Katoliki na kusali sala ya kuombea miito mitakatifu ili kanisa liweze kuendelea kuwa imara daima.
Askofu Mapunda amewashukuru wazazi wa Padre Paterni kwa malezi bora kwa watoto wao hatua ambayo imemfanya Padre huyo kujitoa kulitumikia taifa la Mungu na kufanya utume wake vema katika kazi anazopangiwa katika kanisa ndani na nje ya jimbo Katoliki la Singida kwa uchaji kadiri Mungu alivyomjalia karama mbalimbali.
Hakika Padre Dkt. Paterni Mangi anapomshukuru Mungu kwa utume wake akiwa katika Parokia ya Mandewa ambapo yeye ndiye paroko wa Parokia hiyo, Dekano wa Dekania ya Kaskazini na Paroko wa Parokia ya Nduguti Padre Stephano Sinda ambaye alitoa homilia takatifu alibainisha talanta lukuki alizojaliwa Padre Dkt. Paterni kwa utume wake tangu akiwa Mseminari mdogo katika Seminari ya Mt. Patrisi Dung’unyi iliyopo Jimbo Katoliki la Singida.
Talanta ni kipaji ama zawadi anayopewa mtu kadiri anavyopenda Mungu ili mwanadamu aliyepewa zawadi hiyo aweze kumtumikia katika maisha yake hatimaye aweze kumtukuza Mungu kupitia kazi anazozifanya mwanadamu huyo kwa watu wengine.
Padre Sinda alisema Dkt. Paterni ni kuhani ambaye amepewa talanta lukuki ambazo ni mali ya Mungu aliyopewa kwa ajili ya kuwatumikia watu wake. Hakika hii ni karama anayoifanyia kazi mwanadamu ili kumletea Mungu faida.
Mtume Paulo katika barua yake kwa Waebrania (1 Waebrania 5:1-4) anabainisha sifa za Kuhani Mkuu ambapo anasema “Kila Kuhani Mkuu hutwaliwa miongoni mwa watu, kwa ajili ya watu lakini kwa mambo ya mhusuyo Mungu,” Padre Sinda anasisitiza huku ndiko kuwekwa Wakfu kwa ajili kumtumikia Mungu na wanadamu.
Padre Sinda anasema vipaji alivyopewa Padre Dkt. Paterni na Mungu baadhi yake ni kujishughulisha, kujibidisha na kuzingatia muziki mtakatifu tangu akiwa Mseminari mdogo katika Seminari ya Mt. Patrisi Dung’unyi na wakati wote hadi sasa anapenda sana muziki huo.
“Hiki kipaji cha muziki mtakatifu ameanza kukitumia tangu akiwa mdogo, anakipenda mno na anakiishi, amefundisha sehemu mbalimbali wanamuziki na watu wengi wamebobea kwa sababu walipata ujuzi kutoka kwake na yeye mwenyewe ametunga nyimbo nyingi tu. Ametumia kipaji alichopewa na Mwenyezi Mungu vizuri kwa ajili ya ufalme wa Mungu na amelitajirisha kanisa na taifa la Mungu kwa Muziki Mtakatifu” alisema Padre Sinda.
Kipaji kingine alichonacho Padre Paterni anapenda sana kufundisha. Wakati alipokuwa ametumwa kufanya kazi ofisi ya Baraza la Maaskofu (TEC) alifanyakazi ya kufundisha katika Seminari Kuu ya Segerea na katika kufundisha kwake anapenda sana kusisitiza uchaji wa Mungu katika ibada na kuishi kadiri ya utaratibu uliyowekwa na kanisa Katoliki.
Ili ibada iweze kufanyika katika mazingira ya Mungu kupewa sifa, Padre Paterni alipopangiwa kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia ya Mt. Joseph Mfanyakzi Mandewa ameendelea kutumia kipaji chake vema kwa kuweka mazingira mazuri ya kujenga nyumba ya Ibada ambapo amefanikiwa kuthubutu kutumia kipaji chake na kushawishi uongozi wa Parokia kujenga kanisa kubwa lenye uwezo wa waumini 2500 kwa wakati mmoja hatua inayosaidia Mungu kupewa sifa ambapo hadi sasa lipo kwenye hatua ya kupaua.
“Hivyo, anamshuru Mungu kwa mambo ambayo Padre Paterni amejaliwa kuyafanya na sisi tumekuja kumshangilia na kumshuru Mungu Mwenyezi pamoja naye kwa mambo ambayo anamsaidia kuyafanya. Paterni hana majivuno anajitahidi katika hali ya uchaji, unyenyekevu na upole kuyafanya yale yote ambayo amekabidhiwa na kuyatenda kwa kadiri ya uwezo wa Mwenyezi Mungu” alisema Padre Sinda.
Vile vile Padre Paterni anakipaji pia cha ukarimu, anajitahidi kujenga mahusiano na watu mbalimbali ili kusudi shughuli za uinjilishaji ziweze kwenda vizuri ndiyo maana anamshukuru Mungu kwa miaka 25 ya utume wake na anaendelea kumwomba Mungu ampe nafasi ili kazi anazokabidhiwa na talanta alizopewa aendelee kuzitumia kuandaa taifa la Mungu liweze kurithi ufalme wa Mungu.
Nao wanamuziki mtakatifu wa kanisa Katoliki wakiongozwa na Mwalimu Fidelis Kashumba na Peter Anton Mavunde kutoka Jimbo Kuu la Dodoma wamesema Dkt. Paterni anauthamini muziki mtakatifu wa Ijili na ameweka alama katika kanisa Katoliki kwa kuliwezesha Baraza la Maaskofu kurasimisha muziki huo mtakatifu hatua inayoendana na maneno ya Mt. Agustino kwamba “anayeimba vizuri anasali mara mbili” ili Mungu atukuzwe na wanadamu wapate utakatifu.
“Umeuthanini utume wa uimbaji, wewe ni mfano hai wa waimbaji kwa kuleta ujumbe kwa waumini, na umeweka dhana njema ya kuwa kuimba sio kupoteza muda” alisema Mwalimu Mavunde.
Huku Mjumbe wa Kamati ya Muziki Mtakatifu Taifa na Mwanakamati ya Muziki Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Fidelis Kashumba akibainisha kuwa Padre Paterni amekuwa na mchango katika kuwezesha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kurasimisha uimbaji ndani ya kanisa Katoliki na kutambua kwaya kama utume ndani ya kanisa Katoliki ambapo katika umoja wao wa Utume wa Kwaya Ndani ya Kanisa Katoliki Tanzania (UKWAKATA) wakiongozwa na kaulimbiu ya “Tumwimbie Bwana katika Roho na kweli” wanauthamini muziki huo na wataendelea kuufundisha ili Mungu atukuzwe daima.
“Kwa hiyo kutokana na kazi alizozifanya kutokana na utaalamu wake wa kilitrujia alianza kazi ya kutuelimisha sisi wanakwaya wanamuziki kuelewa maana ya muziki mtakatifu kama unavyoelekezwa na mama kanisa katika maandiko yake” alisema Mwalimu Kashumba.
katika kuthamini kazi ya muziki mtakatifu ambayo anaifanya Padre Paterni, Wanamuziki mtakatifu walimuunga mkono na kushiriki pamoja naye misa ya shukrani ya iliyofanyika Oktoba 15 na 17, 2020 ya kumshukuru Mungu kwa Jubilei ya Fedha katika utume wake.
Wanamuziki mtakatifu hao ni Fidelis Kashumba, Peter Mavunde na Zakaria Blackman kutoka Dodoma, Lukas Mlingi kutoka Arusha, Damas Malya, Jerry Newman, Lazaro Patiu, Fredy Patiu, Casmir Gilishi, Francis Ndojekwa, Adventina Elias wote kutoka Dar es Salaam pamoja na wanakwaya 60 kutoka Parokia ya Igunga Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Mt. Joseph Mfanyakazi Mandewa Martin Magagura ametaja mambo ambayo Padre Patreni amekuwa mstari wa mbele ni pamoja na mahubiri yake ambayo yanaendelea kuwakomaza waumini kiimani, kuwajenga na kuwahimiza waumini kuwa na moyo wa majitoleo kwa mambo ya kanisa ambapo hatua hiyo imewasaidia waumini parokiani humo na ushirikiano wa pamoja na kuwa wamoja wenye amani na upendo.
Kuhusu uhai wa kanisa, Parokia ya Mandewa inaendelea kusonga mbele katika kuijilisha na kulea imani ambapo wakati Parokia hiyo inazinduliwa ilikuwa na vigango 16 wakati kwa sasa vipo vigango 20, visinagogi vinne pamoja na jumuiya ndogondogo 34 wakati awali kulikuwa na jumuiya 16.
Fauka ya hayo, Parokia ya Mandewa inaendelea kuimarika pia katika sakramenti mbalimbali za kanisa ambapo kwa kipindi cha miaka mitano tangu kufunguliwa kwake na Mhashamu Askofu Edward Mapunda Oktober 17, 2015 ikiwa na waumini 4606 na sasa idadi ya waumini imefikia 4800.
Aidha, hadi sasa waumini 1245 wamebatizwa, waumini 379 wamepata kumunyo ya kwanza, waumini 714 walipata sakramenti ya Kipaimara na idadi ya waumini walipoata Sakramenti ya ndoa ni 89.
Katika shughuli za maendeleo, Padre Patreni amekuwa mstari wa mbele katika shughuli za parokia hiyo ikiwemo uboreshaji wa nyumba ya mapadre, ujenzi wa kanisa la Parokia ambalo lipo katika hatua ya kupaua, ujenzi wa makanisa ya kisasa katika vigango nane ambayo yapo katika hatua mbalimbali pamoja na ujenzi wa madara na bwalo katika shule ya msingi Upendo inayosimamiwa na Parokia hiyo.
Mapadre waanzilishi waliohudumia Parokia hiyo ni Padre Paterni Mangi akiwa Paroko na Padre Lucas Kinanda akiwa Paroko Msaidizi. Kwa sasa Parokia inahudumiwa na Mapadre watatu ambao ni Padre Paterni Mangi ambaye amekuwa Paroko tangu kuanzishwa Parokia hiyo hadi sasa, Padre Raphael Madinda na Padre James Ngoi.
Padre Dkt. Paterni Mangi alizaliwa Aprili 16, 1966 katika kijiji cha Mvae wilaya ya Singida (V) mkoani Singida akiwa mtoto wa sita kuzaliwa katika familia ya Katekista Patrisi Mangi na Marehemu Teresia Bonifasi.
Padre Dkt. Paterni Mangi alianza safari yake ya elimu katika shule ya msingi Mvae kuanzia 1975 hadi 1981, alipata elimu yake ya sekondari katika Seminari ya Mt. Patriki Dung’unyi mwaka 1982 hadi 1985, alisoma kidato cha tano na sita katika Seminari ndogo ya Rubya iliyopo jimbo la Bukoba mwaka 1986 hadi 1988, alisoma masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Mt. Antoni iliyopo Ntungamo Jimbo Katoliki la Bukoba mwaka 1988 hadi 1990 na , alisoma masomo ya Theolojia katika Seminari Kuu ya Kipalapala iliyopo Jimbo Kuu la Tabora mwaka 1990 hadi 1995.
Katika utume wake amehudumia sehemu mbalimbali ikiwemo Parokia ya Mtinko kati ya mwaka 1995 hadi 1999, alifundisha kama mwalimu katika Seminari ndogo ya Mt. Patrisi Dung’unyi kati ya mwaka 1999 hadi 2000, Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Singida kati ya mwaka 2000 hadi 2004, alikwenda masomoni huko Roma Italia kwa masomo ya Uzamili na Uzamivu kati ya mwaka 2004 hadi 2012 na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Litrujia.
Aidha, kati ya mwaka 2012 hadi 2014 alipangiwa kufanyakazi katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika Kurugenzi ya Litrujia na wakati huo huo alikuwa Mhadhiri na kufundisha katika Seminari Kuu ya Segerea iliyopo jimbo kuu la Dar es Salaam.
No comments: