MAJALIWA: TUMCHAGUE DKT. MAGUFULI SI MLALAMISHI
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akiwaomba wananchi wa Kigoma wampigie kura mgombea urais wa CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mwanga Centre mjini Kigoma
……………………………………………………………..
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa Kigoma wahakikishe wanamchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwa sababu ni kiongozi shupavu, mpenda maendeleo na si mlalamishi.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Oktoba 18, 2020) alipozungumza na wakazi wa Kigoma kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Mwanga Centre wakati akimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda na wagombea udiwani wa CCM.
“Tumchague Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi tunayemjua na ametumikia katika nafasi ya urais kwa ufanisi mkubwa. Dkt. Magufuli ameweza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, barabara na maji katika kipindi cha muda mfupi wa miaka mitano, tumpe ridhaa ya kuongoza miaka mitano mingine ili tupate maendeleo zaidi.”
Amesema CCM ndio chama pekee chenye dhamira ya kuwaletea maendeleo na wasifanye makosa kwa kuchagua wagombea wasiokuwa na uwezo wa kuwatumikia na badala yake wachague wagombea kutoka CCM kwani ina ilani ambayo imeorodhesha miradi yote ya maendeleo itakayotekelezwa nchi nzima ikiwemo na Kigoma.
Amesema wananchi wanatakiwa wamchague Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi muadilifu, mchapakazi na mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu na upendo kwa watu wa dini zote na anauwezo wa kusimamia kazi ipasavyo na ndio sababu Tanzania sasa inamaendeleo makubwa. “Oktoba 28 mwaka huu nendeni mkamchague Dkt. Magufuli.
Akizungumzia kuhusu miradi ya ujenzi wa barabara iliyotekelezwa Kigoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. bilioni 63.323 kwa ajili ya ujenzi barabara kutoka Kidahwe hadi Kasulu kwa kiwango cha lami na tayari mradi huo umekamilika na utanufaisha maeneo ya Wilaya za Kasulu na Kigoma.
“Serikali imetoa shilingi bilioni 47.159 kwa ajili ya mradi wa ujenzi barabara kutoka Nyakanazi hadi Kabingo yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami, ambapo kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 86 na utanufaisha maeneo ya Wilaya ya Kakonko.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema miradi mingine ya barabara za mkoa wa Kigoma ambazo zimetengewa fedha katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2020/2021 ni pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Manyovu – Kasulu – Kabingo, shilingi bilioni 372.109 zitatumika kujenga kilomita 260.6 kwa kiwango cha lami.
Awali, katika kuonyesha kuwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma wamechoshwa na upinzani wanachama 200 wa Vyama vya Upinzani wengi wao kutoka ACT Wazalendo wakiongozwa na aliyekuwa meneja wa kampeni wa Zitto Kabwe, Patrick Mzigama wamekihama chama hicho na kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na kasi kubwa ya maendeleo iliyofanywa na serikali ya CCM katika awamu ya kwanza ya Uongozi wa Rais Dkt. Magufuli.
Mzigama ametumia fursa hiyo kuwaomba radhi wakazi wa Kigoma Mjini kwa sababu yeye ndiye aliyewaongoza katika kuchagua vibaya mwaka 2015, hivyo amewaomba wabadilike na siku ya kupiga kura itakapofika wakawachague wagombea wote wa CCM. “Rais Dkt. Magufuli amejenga miradi mikubwa na maendeleo, amerudisha nidhamu kwa watumishi wa umma na wanafunzi wanasoma bure hivyo hatuna sababu ya kumchagulia mtu ambaye hawataongea lugha moja.”
No comments: