KUSAYA: TUTAIJENGA SKIMU YA UMWAGILIAJI NGUVUKAZI MWANAVALA MBARALI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (aliyevaa fulana nyekundu) akiongea na wakulima wa mpunga Mwanavala wilaya ya Mbarali jana alipotembelea kukagua miundombinu yao ya asili ya umwagiliaji.Kusaya ameahidi kuwa mara baada ya kutekelezwa kwa magizo ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuhusu kurasimisha maeneo yaliyokuwa ndani ya hifadhi,wizara yake itajenga miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ( aliyevaa tshirt nyekundu) akitazama banio na mfereji wa kienyeji wa umwagiliaji unaotumiwa na wakulima zaidi ya 3500 wa Nguvukazi Mwanavala kuzalisha mpunga wilayani Mbarali jana alipofanya ziara ya kikazi.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akiwa kwenye banio la umwagiliaji Nguvukazi Mwanavala akiongea na wakulima wa mpunga jana kufuatia ziara yake ya kikazi kwenye mashamba hayo.Katibu Mkuu Kusaya amewataka wakulia hao waendelee kulima kwa amani wakati suala la urasimishaji eneo hilo ukiendelea na kamati ya mawaziri.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akitazama mashamba ya wakulima wadogo wa mpunga katika bonde la mto Ruaha kijiji cha Nguvukazi Mwanavala wilayani Mbarali jana alipotembelea kukagua miundombinu ya mashamba hayo yenye ukubwa wa hekta zaidi ya 6,500.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (mwenye tshirt nyekundu) akiwa na wakulima wa mpunga kijiji cha Ubaruku Mbarali jana alipotembelea kiwanda chao cha kukoboa mpunga ambapo ameahidi serikali itawasaidia kutafuta masoko ya mchele.

 

Wakulima wa mpunga bonde la mto Ruaha wilayani Mbarali wakiwa na Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya jana alipofanya ziara ya kikazi kwenye eneo hilo linalokadiriwa kuwa na hekta 9,500 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo)

………………………………………………………………………………..

Wizara ya Kilimo imesema itajenga miundombinu ya skimu ya umwagiliaji katika kata ya Imalilo Songwe wilaya ya Mbarali yenye eneo linalokadiriwa kuwa hekta 6,500 baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa maagizo ya Rais kupitia kamati ya mawaziri.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati akiongea na wakulima wa mpunga wa skimu ya umwagiliaji ya Nguvukazi Mwanavala wilayani Mbarali  akiwa ziarani kukagua shughuli za kilimo.

Kusaya aliwataka wakulima wa skimu hiyo inayolimwa kwa kutumia miundombinu ya kienyeji takribani hekta 6,500 kati ya eneo lote linalofaa kwa umwagiliaji la hekta 9,500 toka mto Ruaha kijiji cha Songwe/ Ibumila ambapo wakulima wamejenga banio la asili.

“Nataka ninyi watu wa Ubaruku na kijiji cha Nguvukazi Mwanavala kitongoji cha Mnazi mfanye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji na cha kibiashara ili tupate mabilionea wengi baada ya skimu hii kujengwa miundombinu ya kisasa na serikali yenu kama alivyoagiza Rais Dkt.John Pombe Magufuli hivyo endeleeni kulima hapa bila hofu” alisisitiza Kusaya

Akiwa kijijini hapo Katibu Mkuu huyo alitembelea mashamba ya wakulima, kukagua mfereji mkuu uliochimbwa na wakulima wenye urefu wa kilometa 8 na pia alitembelea kiwanda cha kukoboa mpunga cha Ubaruku kinachoendeshwa na ushirika wa wakulima hao na kuahidi kutatua changamoto za upatikanaji soko la mchele.

Akijibu risala ya wakulima kuomba kupatiwa msaada wa kujengewa mtaro wa kisasa wa umwagiliaji, Kusaya aliwataka wawe na subira wakati kamati ya mawaziri ikiendelea kutekeleza agizo la Rais kuhusu kurasimisha vijiji 975 vilivyopo ndani ya hifadhi ili vitambulike na kuwa maeneo ya kilimo na ufugaji.

“Wakulima kuweni na subira tumalize kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli ikiwemo kutambua mipaka ya kijiji na hifadhi kisha nitawatuma wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuja hapa Ubaruku kufanya upembuzi yakinifu ili tuijenge skimu hii kisasa na kuweza kuongeza tija ya uzalishaji mpunga” alisisitiza Kusaya.

Lengo la wizara ya kilimo ni kujenga miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima Mwanavala ili maji yasipotee bure alisisitiza Kusaya na kuongeza kuwa watalaam wa Tume ya Taifa ya umwagiliaji watahusika kufanyaka kazi hiyo baada ya maagizo ya Rais kutekelezwa. 

Akitoa tarifa ya ushirika wa shamba la Nguvukazi Mwanavala Katibu wa kikundi hicho Christopher Uhagile alisema ushirika huo ulianza mwaka 2002 na kuwa sasa wana wanachama 3,500 wanaolima mpunga katika mfereji licha  ya miundombinu kutokuwa ya kisasa.

Akizungumzia changamoto za kubomolewa kwa banio la mfereji wa umwagiliaji mwaka 2018 na mwekezaji hali iliyoyasabisha mgogoro na wakulima lakini wanashukuru uamuzi wa Rais kuagiza banio hilo kujengwa na wakulima waruhusiwe kutumia maji.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Jonh Pombe Magufuli kwa maelekezo yake ya tarehe 20.12.2018 kusema tuendelee kulima eneo hili na kuwa banio na mfereji wetu ufukuliwe na kujengwa na kuwa tusisumbuliwe tena sasa limetekelezwa na uongozi wa mkoa na wilaya” alisema Uhagile

Naye mwakilishi wa wakulima Chubi Mbayinjini wa kitongoji cha Mnazi alisema wanashukuru uamuzi wa Rais Magufuli kuondoa GN 28 haki inayowafanya waendelee na kilimo katika mashamba ya Mwanavala.

Alitoa wito kwa uongozi wa bonde la mto Ruaha ili waruhusu kibali cha kutumia maji hayo kunusuru mazao ya wakulima kipindi cha ukame na kuwezesha uzalishaji mpunga kuongezeka zaidi.

Mbayinjini alisema wamekuwa wakifuatilia kibali cha kutumia maji ya bonde la mto Rufiji tangu mwaka 2001 bila majibu toka kwa wahusika hali inayowakatisha tamaa wakulima kuzalisha zaidi mpunga.

Katibu Mkuu Kusaya kufuatia ziara yake kwenye mashamba hayo ya mpunga ya wakulima wadogo Mwanavala aliridhishwa na kazi wanayoifanya na kuahidi kushirikiana na makatibu wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara naile ya Maji ili wafanye utatuzi wa changamoto za masoko ya mchele na kibali cha utumiaji maji.

Kusaya alitoa rai kwa Viongozi wa mkoa wa Mbeya na wilaya kuweka mazingira mazuri kwa wakulimakupenda kufanya kazi za kilimo ili nchi ijitosheleze kwa chakula na wakulima wapate kipato chao kukuza uchumi wa kaya na taifa.

Katika hatua nyinie Kusaya alitembelea na kuongea na uongozi wa shamba la mpunga la Mbarali Highland Estate na kukitaka kianzishe kiwanda chake cha mbolea ili kupunguza utegemezi wa mbolea toka nje ya nchi hali inayopunguza uzalishaji.

Katibu Mkuu Kilimo yupo kwenye ziara ya mikoa ya Mbeya,Songwe,Rukwa na Katavi kukagua shughuli za wakulima na kuongea na watendaji waliopo chini ya wizara ya kilimo kutatua changamoto za sekt hiyo ikiwemo umwagiliaji.

No comments: